Uhamasishaji madawati ya kijinsia vyuoni waanza

24Nov 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Uhamasishaji madawati ya kijinsia vyuoni waanza

SIKU 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka huu zinaadhimishwa kwa kuhamasisha uanzishwaji wa madawati ya kijinsia vyuoni.

Madawati hayo yatasaidia wanafunzi wanapokutana na ukatili kupeleka malalamiko yao na hatua kuchukuliwa.

Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF), Anna Kulaya, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika mafunzo ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na shirika hilo na wadau wengine  na kutolewa kwa wahariri na waandishi wa habari.

Kulaya alisema maadhimisho ya mwaka huu watayatumia kupita mikoa mbalimbali wadau ikiwamo vyuoni kutoa elimu kuhusu kuanzishwa kwa madawati hayo.

Alisema takwimu zinaonyesha kati ya matukio 11,726 yaliyoripotiwa, matukio ya ubakaji ni 7,617 sawa na asilimia 64. 

Akizungumza katika mafunzo hayo, Kulaya alisema maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika kwa kuwa na matukio tofauti ikiwamo misafara itakayopita maeneo mbalimbali mikoani na kwenda vyuoni ili kuhakikisha kunaanzishwa madawati maalum ambayo yatawezesha wanaofanyiwa vitendo hivyo kupeleka malalamiko yao.

"Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeonyesha asilimia 50 ya waliohojiwa wameeleza rushwa ya ngono vyuoni.

"Ndiyo maana katika maadhimisho ya mwaka huu yaliyobebwa na kauli mbinu isemayo, 'Tupinge ukatili wa kijinsia mabadiliko yanaanza na mimi' tumeona pamoja na mambo mengine tuende vyuoni kuzungumza nao pindi wanapokutana na vitendo hivyo wachukue hatua ya kutoa taarifa."

Alisema baada ya mafunzo hayo yaliyotolewa kwa wahariri na waandishi wa habari, Jumatano itakuwa ni Siku ya Kimataifa ya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Aliongeza kuwa ndani ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kutakuwa na tuzo kwa wanawake 16 waliotoa maisha yao kutetea wanawake wengine.

Kadhalika, alisema wataangalia ukatili wa kijinsia unaotokea nyumbani kwa sababu ni moja ya maeneo ambayo yanatakiwa kuwa salama.

Vilevile, alihimiza jamii kuhakikisha inapaza sauti na kufanya mabadiliko maeneo yao.

Mkuu wa Mawasiliano serikalini kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii), Prudence Constantine, alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa sasa vimevuka mipaka na sasa kuna ukatili wa kisaikolojia unaowahusisha jinsia zote, lakini taarifa zake siyo za kutosha.

"Serikali imechukua hatua mbalimbali ya kutokomeza vitendo hivi. Upo mpango wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, tunampango wa kupunguza ukatili kwa asilimia 50.

"Yapo madawati ya kijinsia 450 yaliyoanzishwa vituo vya Polisi kwa ajili ya kupokea taarifa za ukatili wa kijinsia, waathirika  58,059 wamejitokeza  kutoa taarifa."
Pia alisema magereza nao wameanzisha madawati 162 nchini.

Ofisa Mtendaji wa Taasisi ya Msaada wa Kisheria (LSF), Lulu Ng'wanakilala, alisema mikakati ni kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia nchini na siyo kupunguza.

Habari Kubwa