Uhamiaji yachukua maelezo ya Kabendera

01Aug 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Uhamiaji yachukua maelezo ya Kabendera

IDARA ya Uhamiaji imesema imeshachukua maelezo ya mwandishi wa habari za uchumi, Erick Kabendera ambaye wanamshikilia kwa uchunguzi kuhusu uraia wake.

Kamishna wa Uraia na Hati za Kusafiria wa Idara ya Uhamiaji, Gerald Kihinga.

Kamishna wa Uraia na Hati za Kusafiria wa Idara ya Uhamiaji, Gerald Kihinga, alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari.

“Tulipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusu utata wa uraia wake, baada ya idara kupata taarifa tulianza kuzifanyia kazi, hata hivyo Kabendera hajawahi kuhojiwa kuhusu uraia wake pamoja na kutumiwa barua ya wito mara nyingi,” alisema.

Kihinga alisema idara yao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ilimtafuta na kumpata na jana (leo) walikuwa naye wakimhoji kuhusu utata wa uraia wake.

Alisema uhakiki wa uraia wenye utata umekuwa ukifanywa kwa watu mbalimbali wakiwamo watu mashuhuri.

“Suala hili limekuwa kubwa kwa sababu Kabendera ni mwandishi wa habari, lakini tuna watu wengi ambao tunawahoji, ingekuwa maadili yanaruhusu ningewatajia watu tunaowahoji kwasababu wapo wengi hata nikiwasema hapa mnaweza kushangaa,” alisema.

“Lakini hatujaweka wazi kwa sababu watu hawa siyo wakukimbia, wamekuwa wakitoa ushirikiano kila tunachowaambia walete wanaleta tofauti na Kabendera. Idara ya Uhamiaji imekuwa ikishirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama katika kutekeleza majukumu yake, suala hili siyo geni,” alisema.

Aliomba jamii kuendelea kutoa ushirikiano na kutoa taarifa mbalimbali pale wanapoona kuna utata wa uraia kwa mtu.

Kamishna Kihinga alisema, Kabendera hajawahi kukamatwa na hiyo ni mara yake ya kwanza.

Kuhusu muda ambao watamshikilia, alisema itategemea na ushirikiano wa mhusika kwa sababu wanapomwita mtu na akatoa ushirikiano wa kupeleka wanavyovihitaji, uchunguzi huisha mapema.

“Kama hutupi ushirikiano suala hilo huchukua muda mrefu na wakati mwingine huwa tunavuka mipaka tunakwenda nchi nyingine kufanya uchunguzi, lini tutamaliza itategemeana na ushirikiano atakaotoa mhusika,” alisema.

Alisema hadi jana walikuwa wameshachukua maelezo yake na taarifa ambazo walikuwa wamezikusanya ili waanze uchunguzi.

“Kuna baadhi ya vitu tulimwomba atuletee, ameahidi atatuletea leo (jana) kama atafanya hivyo atakuwa ameturahisishia sana uchunguzi wetu. Tunapomchunguza mtu hatuangalii rangi, sura, mamlaka aliyonayo au kazi, tunachunguza uraia,” alisema.

Alisema wao wanatumia njia ya kumwita mtu ili kumhoji, lakini akikataa wanakwenda kumkamata na kwamba Kabendera aliwahi kutuhumiwa kwamba siyo raia wa Tanzania mwaka 2013.

Alisema amekuwa akiitwa mara kadhaa bila kufika kwa ajili ya mahojiano na walipokwenda kumkamata walivaa kiraia ili isiwe rahisi kwao kutambulika.

Habari Kubwa