Uhamiaji yakalia pasi bosi Twaweza miezi 4

16Dec 2018
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Uhamiaji yakalia pasi bosi Twaweza miezi 4

IDARA ya Uhamiaji bado inaendelea kuishikilia hati ya kusafiria ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Twaweza, Aidan Eyakuze, kwa miezi minne sasa ikisema inaendelea na uchunguzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Twaweza, Aidan Eyakuze, picha mtandao

Mmoja wa maofisa wa Twaweza ambaye aliomba asitajwe jina, aliiambia Nipashe jana kuwa wamejitahidi kufuatilia kwa muda mrefu lakini wameshindwa kuipata na majibu ni kwamba uchunguzi unaendelea.
 
Alisema wamekuwa wakiandika barua mbalimbali wakiomba kupatiwa hati hiyo lakini idara hiyo imekuwa ikiwajibu kuwa inaendelea na uchunguzi ingawa haisemi itakamilisha lini.
 
Ofisa huyo alisema Mkurugenzi huyo hajasafiri nje ya nchi tangu hati yake ishikiliwe Julai 24, mwaka huu, hivyo amekuwa akikosa mikutano mbalimbali muhimu ya kimataifa na kikanda.
 
“Sisi tuna ofisi zingine Kenya na Uganda ambako alipaswa kwenda mara kwa mara kwa ajili ya shughuli za kiofisi lakini amekwama kutokana na hati hiyo kuendelea kushikiliwa na Uhamiaji,” alisema.

“Tunaomba mtusaidie kuwauliza Uhamiaji wanachotaka ni nini kwa sababu miezi minne yote hawajachunguza na kupata taarifa wanazotaka au ni kumkomoa mtu jamani?” alihoji ofisa huyo.

Alipozungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Eyakuze alisema hakuelezwa sababu za kushikiliwa kwa hati hiyo.

Eyakuze alisema alipokea wito kutoka Uhamiaji kwamba anatakiwa na baada ya kufika, aliambiwa aandike maelezo na siku ya pili alitakiwa kuwasilisha hati yake ya kusafiria.

“Niliwasilisha hati yangu ya kusafiria kama nilivyotakiwa ingawa sijapatiwa sababu ya kuendelea kushikiliwa kwa hati hiyo hadi leo (jana),” alisema.

Alisema Agosti Mosi, alizuiwa kusafiri kwa kutumia shahada ya dharura iliyotolewa kwa utaratibu uliopo ili aweze kushiriki mikutano ya kikazi kwenye ofisi ya Twaweza jijini Nairobi na Kampala, Uganda.

“Hatuna taarifa ya amri ya Mahakama yenye kuidhinisha jambo hili,” alisema Eyakuze.

Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda, alipotafutwa wakati huo alithibitisha kushikiliwa kwa hati ya Eyakuze na kueleza kuwa wanaendelea na upelelezi kujua uraia wake.

Alisema kama watabaini kuwa si raia halali wa Tanzania, atatakiwa kufuata utaratibu wa kupata kibali cha kuishi nchini na kama atakuwa raia atarudishiwa hati yake.

Jana, Nipashe ilifanya jitihada za kumtafuta Mtanda ili kujua uchunguzi huo umefikia wapi na wanatarajia kuachilia hati hiyo lini lakini mara kadhaa alipopigiwa hakupokea simu.

Aidha, Eyakuze alisema Twaweza imepitia kipindi chenye changamoto za ushirikiano baina yake na baadhi ya taasisi za serikali kutokana na uzinduzi wa taarifa za ripoti mbili za Sauti za Wananchi Julai 5, mwaka huu.

“Tumepokea barua mbili kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ambazo zinahoji uhalali wa programu ya Sauti za Wananchi na kututaka tufafanue kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yetu. Tumezijibu barua zote mbili kwa wakati tuliopewa,” alisema.

Habari Kubwa