Uhamisho hakimu wakwamisha hukumu ya Malinzi

08Nov 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Uhamisho hakimu wakwamisha hukumu ya Malinzi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepiga kalenda kutoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo kutakatisha fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake watatu mpaka Novemba 21, mwaka huu.

Aliyekuwa rais wa shirikisho la soka nchini (TFF) Jamali Malinzi akiwa chini ya ulizi wa askari magereza akitoka kusikiliza kesi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. PICHA: MIRAJI MSALA

Hukumu hiyo ilipangwa kusomwa jana, lakini kwa kuwa Hakimu Mkazi, Maira Kasonde, aliyesikiliza kesi hiyo kuhamishiwa kituo kingine cha kazi.

Kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi, Kevini Mhina.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Pendo Temu, alidai kuwa kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Kasonde, lakini upande wa Jamhuri umepata taarifa kwamba amehamishiwa kituo kingine cha kazi.

"Mheshimiwa upande wa Jamhuri tumepata taarifa kwamba Hakimu Kasonde amehamishiwa kituo kingine cha kazi tunaomba mwongozo wa mahakama," alidai Temu.

Hakimu Mhina alisema ni kweli Hakimu Kasonde amepata uhamisho na taratibu za kumwezesha kuandika hukumu hiyo zimekamilika na itasomwa Novemba 21, mwaka huu.

Mapema mahakamani hapo upande wa Jamhuri uliita mashahidi 15 na vielelezo tisa kuthibitisha kesi hiyo na utetezi wanne kupangua tuhuma hizo.

Mbali na Malinzi, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa, Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani Flora Rauya.

Katika kesi hiyo mashahidi 15 wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi na tayari aliyekuwa Rais wa TFF Jamal Malinzi ameanza kujitetea mahakamani hapo.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 washtakiwa Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha kuwa miongoni mwa mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku Flora akiwa nje kwa dhamana.