Uharibifu misitu watishia usalama

14Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Mbeya
Nipashe Jumapili
Uharibifu misitu watishia usalama

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Hassan Chande, amesema uharibifu wa misitu nchini umekuwa mkubwa na hivyo kutishia usalama.

Akizungumza juzi jijini Mbeya katika uzinduzi wa mradi wa urejeshwaji endelevu wa mazingira na hifadhi ya bioanuai, Chande alisema utafiti umebainisha kila mwaka nchi hupoteza wastani wa takribani hekta 469,420 za misitu na kusababisha upotevu mkubwa wa bioanuai inayochangia hatari ya kutoweka kwa baadhi ya aina muhimu za jamii ya mimea na wanyama.

“Kama kasi ya uharibifu wa mazingira isipodhibitiwa, nchi yetu itakuwa katika hatari ya kugeuka jangwa. Kwa mfano, tathmini iliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii imeonyesha hali ya uharibifu ikiendelea hivyo katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2033, uharibifu wa misitu utaigharimu serikali kiasi cha Sh. bilioni 167 za kurejesha mazingira katika hali yake. Kiasi hiki kingeweza kufanya shughuli za kimaendeleo katika taifa letu kama tutatunza mazingira vizuri.” alisema.

Chande alisema kuwa nchi inakadiriwa kuwa na hekta millioni 48.1 za misitu, sawa na wastani wa asilimia 51 ya eneo lote la nchi kavu ambayo ina manufaa makubwa katika hifadhi ya bionuai ikiwamo makazi ya viumbe hai na vyanzo vya maji, ambavyo husaidia kupunguza joto ukaa na zaidi husaidia kutunza ardhi na kuifanya kuwa na rutuba.

“Serikali haitavumilia kuona ubadhilifu wa aina yoyote katika utekelezaji wa mradi huu na kwa Ofisi ya Makamu wa Rais itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha thamani ya fedha inaendana na miradi itakayotekelezwa katika maeneo yetu,” alisema.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga, alibainisha kuwa mradi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 11.2, sawa na Sh. bilioni 25.7.

Alisema lengo la mradi huo ni kuimarisha usimamizi wa pamoja wa mazingira na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibika ili kuleta ustawi wa mifumo ikolojia na jamii kwa ujumla na ni sehemu ya mradi mkubwa wa kidunia (The Global Groject) unaotekelezwa katika nchi 11 duniani ikiwamo Tanzania.

Maganga alishukuru GEF na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa kushirikiana na serikali kupata fedha za utekelezaji wa mradi huo na Shirika la IUCN kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais katika hatua zote za maandalizi ya mradi.

Habari Kubwa