Ujangili meno ya tembo wadhibitiwa kaskazini

24Jun 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Ujangili meno ya tembo wadhibitiwa kaskazini

UJANGILI wa meno ya tembo ukanda wa kaskazini umekwisha, na sasa wanaokufa hukutwa na meno yao tofauti na miaka ya nyuma ambako ujangili ulishamiri.

Hayo yalibainika mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya waandishi wa habari 10 wa Tanzania na Thailand, walioko kwenye programu maalum ya kuandika habari za ujangili na uhifadhi, chini ya Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania, kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

Akiwasilisha mada ya hali ya ujangili na namna wanavyokabiliana na ujangili kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga, Kamanda wa Kikosi dhidi ya Ujangili Kanda ya Kaskazini-Arusha, Peter Mbonjoko, alisema jitihada za serikali ya awamu ya tano zimezaa matunda hayo.

Alisema data za mwaka 2018 zinaonyesha kuwa tembo 12 walikufa kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni wasiojulikana chanzo cha kifo inawezekana kuwa ni umri mkubwa (7), aliyeuawa kutokana na kuua mtu (1) na ugonjwa wa kimeta (4).

Aidha, tembo 22 waliokolewa kwa kupewa tiba mbalimbali na kwamba kwa wote mizoga yao ilikutwa ikiwa na meno yake yote, jambo ambalo ni kiashiria kuwa kwa sasa hakuna ujangili.

“Miaka mitatu iliyopita ilikuwa ni ngumu sana tembo afe alafu ukute meno yake, na ujangili ulishika kasi sana kiasi cha mamia ya tembo kuuawa huku mtandao ukihusisha watu wa ngazi ya chini hadi taifa,” alibainisha.

Alisema takwimu za mwaka 2012 zinaonyesha tembo 64 waliuawa, lakini baada ya serikali kuimarisha vikosi na kuhakikisha taasisi zote zinashirikiana ujangili umeisha.

Kwa mujibu wa Mbanjoko, Julai 2018 hadi mwaka huu, jumla ya watuhumiwa 113 walikamatwa kwa makosa ya kuwinda wanyamapori kwa ajili ya kitoweo na biashara.

Alisema ujangili huo mpya kwa sasa unashika kasi baada ya ujangili wa tembo na faru kupigwa mafuruku na kubomoa mtandao, na sasa watu wanaua wanyama kwa ajili ya kusafirisha nyama nje ya nchi.

Kamanda huyo alisema jitihada zinazofanywa na kikosi kwa kushirikiana na wasamaria wema, ni kumaliza mtandao wa biashara hiyo ikiwa ni pamoja na kesi zote kushughulikiwa ipasavyo.

Alitaja vifaa walivyokamatwa navyo watuhumiwa hao kuwa ni pikipiki (40, nyaya (117), mishale (6), tochi (24), visu (25) na nyara mbalimbali (306) na kesi mbalimbali zinaendelea mahakamani na nyingine zimeshaamuliwa.

Kamanda huyo alisema kati ya watuhumiwa 113 kesi 106 zimeshahukumiwa, 12 zinaendelea kuchunguzwa, tisa zilifika mwisho na tatu watuhumiwa walihukumiwa miaka 5o jela, huku wengine watatu wakiachiwa.

Aidha, faini zilizotozwa ni zenye thamani ya Sh. milioni 74.1 kwa kesi 15, na kwamba kuna kesi 80 zinaendelea kusikilizwa kwenye mahakama mbalimbali ukanda huo.

Habari Kubwa