Ujenzi wa miundombinu Dar wamridhisha Makonda

02Jul 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ujenzi wa miundombinu Dar wamridhisha Makonda

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema kuwa ujenzi wa barabara kilomita 111 kwa kiwango cha lami na kilometa 40 ya mito na mabonde ya kilometa 150, umefikia hatua nzuri.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Sinza, jijini Dar es Salaam, baada ya kufanya ziara ya kukagua miundombinu hiyo, alisema ameridhishwa na ujenzi huo.

Aidha, alisema serikali ilitenga zaidi ya Sh. trilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa barabara, vivuko na kutengeneza mito na mabonde katika Wilaya ya Ubungo na majimbo yake.

“Hizi ni barabara mpya za lami na siyo changarawe wala vumbi, pia kuna kilometa 40 za kutengeneza mito na mabonde kwa ajili ya watoto kuvuka wakati wanapotoka shule,” alisema Makonda.

Alizitaja barabara hizo kuwa ni Kigogo, Aseno Magoti, Kata ya Saranga na Kata ya Kimara ni za Kibanda cha Mkaa, Temboni, Stopover, Suka, Baruti na Kilungule.

Kadhalika alisema anamwamini Rais Magufuli kwa uchapaji wake wa kazi na anatumaini atachukua urais kwa nafasi nyingine kwa ajili kuendelea kuboresha maendeleo ya nchi.

Naye, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, ambaye ni mlezi wa CCM Dar es Salaam, Zakaria Mwasasu, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kusimamia maendeleo ya mkoa huo ambayo yameleta mafanikio katika maisha ya wananchi.

Imeandikwa na Fatma Mtutuma, Faudhia Sultan, UDOM

Habari Kubwa