Ukaguzi mikataba ajira za madereva Julai 15

04Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Ukaguzi mikataba ajira za madereva Julai 15

SERIKALI imetangaza kuwa itafanya ukaguzi wa mikataba ya ajira za madereva ili kuangalia utekelezaji wa Sheria ya Kazi baada ya kubainika baadhi ya kampuni za usafirishaji kufanya udanganyifu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ukaguzi huo utafanyika Julai 15, mwaka huu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani na Mamlaka ya Usafiri wa Ardhi (LATRA).

Taarifa hiyo ilisema kuwa baadhi ya kampuni zinazomiliki vyombo vya usafirishaji zimekuwa zikifanya udanganyifu kwenye mikataba ya ajira, malipo ya mishahara na posho mbalimbali.

“Kwa upande wa utekelezaji wa Sheria za Kazi, changamoto zimeendelea kujitokeza katika masuala ya mikataba ya ajira, malipo ya mishahara na posho mbalimbali ambapo imebainika zipo kampuni chache zinazolenga kuchafua kazi nzuri inayofanywa na sekta hii,” ilisema.

Taarifa hiyo ilisema kampuni hizo chache zimekuwa zikifanya udanganyifu kwenye mikataba ya ajira za madereva wao yanapofanya maombi ya leseni za usafirishaji.

“Katika jitihada za kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo, ofisi yangu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na LATRA tutafanya ukaguzi kwa lengo la kukagua mikataba hiyo na kuangalia utekelezaji wa sheria kwa ujumla,” ilisema.

Aidha, taarifa hiyo iliwataka wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, wafanyakazi, madereva na umma kuhakikisha mikataba ya madereva inakuwapo katika maeneo yao ya kazi.

“Madereva mhakikishe mnakuwa na nakala za mikataba yenu mnapokuwa katika kazi zenu ili iwe rahisi kwa wakaguzi kuiona. Ukaguzi huu ni endelevu na utahusisha pia sekta nyingine nchini,” alisema.

Pia ilisema kuwa katika kutimiza azma ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, serikali inaendelea pamoja na mambo mengine, kuimarisha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara katika sekta mbalimbali ikiwamo ya usafirishaji.

“Sekta hii ni miongoni mwa sekta zenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuongeza mapato ya serikali. Imekuwa ikichangia pia kuzalisha ajira kwa vijana wetu katika nafasi mbalimbali kama vile madereva, mafundi na kada nyingine,” ilieleza.

Taarifa hiyo ilisema kuwa pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na sekta hiyo, zipo changamoto kadhaa ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi na serikali kwa kushirikiana na wadau.

Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kuwa, ukaguzi huo utafanyika kwa namna mbili, maofisa kazi waliopo katika ofisi za kazi kupita katika kampuni zote za usafirishaji na nyingine ni timu maalum ya maofisa kazi wa kushirikiana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi madereva, LATRA na Jeshi la Polisi kukagua mikataba kwenye vituo vikuu vya ukaguzi.

“Vituo hivi ni kama vile kituo cha mabasi Ubungo, kituo cha kuegesha malori cha Misugusugu na vituo vingine vinavyofanana na hivyo hapa nchini,” alisema.

Pia, taarifa hiyo ilieleza kuwa ukaguzi huo utakwenda sambamba na viongozi wa vyama vya wafanyakazi, madereva na vyama vya waajiri kupatiwa elimu kuhusu haki na wajibu wao katika kutekeleza sheria hiyo.

“Napenda kutoa wito kwa wamiliki vyombo vya usafirishaji, viongozi wa vyama vya wafanyakazi, madereva pamoja na madereva wote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakaguzi wakati wote wa ukaguzi, ili kutoathiri utoaji wa huduma kwa wananchi kwa namna yoyote ile,” ilisema.