Ukame wakwamisha wananchi kufunga ndoa

22May 2019
Asraji Mvungi
ARUSHA
Nipashe
Ukame wakwamisha wananchi kufunga ndoa

WANANCHI wanaoishi vijiji vilivyoko pembezoni mwa wilaya za Mbulu mkoani Manyara na Karatu mkoani Arusha, wamelalamikia kuendelea kukabiliwa na umaskini wa kipato unaotokana na kuandamwa na ukame, unaowaathiri kukaa bila kufunga ndoa.

Wananchi hao waliyasema hayo wakati wa ibada maalumu ya kuadhimisha Siku ya Familia, iliyoandaliwa na Kanisa Katoliki Parokia ya Kitete, iliyoko Wilaya ya Karatu mkoani Arusha na waamini zaidi ya 240 kujitokeza kupata huduma ya kufunga ndoa baada ya kanisa hilo kuwalipia gharama za stakabadhi za ndoa.

Wakizungumzia ukubwa wa tatizo hilo, wananchi hao walisema kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo, ambayo ndio tegemeo lao kwa chakula na biashara, uwezo wao wa kutekeleza majukumu muhimu yakiwamo ya kuhudumia familia na maendeleo yamekuwa yakipungua siku hadi siku.

Mmoja wa wananchi hao, Antony Simion, mkazi wa Kijiji cha Kitete, Tarafa ya Mbulumbulu wilayani Karatu, alisema athari ni kubwa zaidi kwa wanawake na vijana, hasa wa kike ambao licha ya kuathirika kiuchumi, pia wanakabiliwa na tatizo kubwa la migogoro ya kifamilia, ambayo huchangiwa na baadhi yao kujihusisha na vitendo vya ulevi.

“Hali inapokuwa ngumu mambo mengi yanakwenda nje ya utaratibu na kiasi kidogo kinachopatikana kimekuwa kikitumika kwa mambo muhimu pekee, mfano kwa sasa wananchi wengi hawataki kufunga ndoa kutokana na fedha kidogo wanayopata kuitumia kwenye mahitaji ya chakula, elimu kwa watoto wao na matibabu na ni masuala ambayo pia ni ya muhimu,” alisema mzee Simion.

Akizungumzia tatizo la watu wengi kuishi bila kufunga ndoa, Paroko wa Parokia hiyo, Sebastian Mwilinga, alisema kwa upande wao wameanzisha utaratibu wa kuzitembelea familia zilizoathirika na kuzipatia elimu na ushauri  nasaha, unaolenga kuwawezesha kudumisha upendo katika familia zao.

Sebastian alisema katika harakati hizo pia walibaini kuwapo kwa tatizo kubwa la watu wengi kuishi kama mume na mke bila kuwa na ndoa, utaratibu ambao umekuwa chanzo cha wanawake na watoto kutekelezwa hasa wakati huu, ambao shughuli za kiuchumi zimeyumba kutokana na ukame.

“Baada ya kuona tatizo hilo tulianza kampeni ya kutoa elimu maalumu ya umuhimu wa kufunga ndoa, ambayo licha ya wengi waokuelewa, bado waliendelea kusingizia kuwa hawafungi ndoa kutokana na ukosefu wa fedha za gharama za ndoa,” alisema Paroko Sebastian.

Alisema katika kutatua tatizo hilo, uongozi wa parokia hiyo ulilazimika kuwaondolea wananchi hao gharama za hati za ndoa na kutangaza siku maalumu ya kufunga ndoa, bila malipo ambayo wananchi zaidi 240 walijitokeza.

Tukio hilo liliongozwa na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbulu, Mhasham Antony Gasper, ambaye licha ya kuwapongeza wanandoa hao, pia aliwasifu viongozi wa parokia hiyo kwa ubunifu ambao ni mfano wa kuigwa maeneo mengine.

Habari Kubwa