Ukarabati uwanja wa ndege wafikia pazuri

19Mar 2019
Hamisi Nasiri
Nachingwea
Nipashe
Ukarabati uwanja wa ndege wafikia pazuri

KAZI ya ukarabati wa mradi wa kiwanja cha ndege kilichopo wilayani Nachingwea, mkoani Lindi wenye thamani ya Sh. milioni 943 umefikia asilimia 75.

Mkandarasi wa mradi huo ambaye ni Kampuni ya Makapo Construction Ltd., amefikia hatua ya G-15.

Utekelezaji wa ukarabati wa kiwanja hicho ni miongoni mwa mpango mkakati wa serikali katika kuboresha viwanja vya ndege nchini ili kuongeza thamani na tija kwenye usafiri wa anga nchini.

Injinia Mkuu wa ujenzi huo, Helifuraha Hema, alisema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa waandishi wa habari waliotembelea kiwanja hicho kuangalia maendeleo ya ujenzi.

Alisema serikali imetoa Sh. milioni 943 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa kiwanja ndege cha Wilaya ya Nachingwea ikiwa ni miongoni mwa mkakati wa kuboresha viwanja vyote vya ndege nchini ili kuboresha usafiri wa anga nchini.

Alisema shughuli za ukarabati na matengenezo ya kiwanja hicho zimefikia asilimia 75 hadi sasa.

Hema alisema serikali imeipa kandarasi ya ukarabati wa kiwanja hicho kampuni ya ujenzi ya Makapo ambayo inajenga kwa kasi kuhakikisha unakamilika ndani ya wakati.

Alisema awali walianza na kazi ya kusafisha uwanja na baadaye kuchimba na kuweka sawa udongo katika viwango vinavyotakiwa kitaaluma kwenye viwanja vya ndege nchini.

Hema alisema kiwanja hicho kupitia ukarabati huo kwa sasa kitakuwa na viwango bora vya viwanja vya ndege utakaokuwa na urefu wa mita 1,800 sawa na kilomita 1.8.

"Tunaihakikishia serikali Kampuni ya Makapo itahakikisha inamaliza mradi huu ndani ya wakati kwa kuwa tumekuwa tukifanya kazi saa zote ili kukamilisha ujenzi huu kama serikali inavyotaka na kutuagiza," Hema alisema.

Alisema serikali imeshatoa muda wa kukamilika kwa mradi huo mwezi Juni, mwaka huu.

Baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo, akiwamo Selemani Mussa, wameipongeza serikali kwa kuamua kutoa fedha hizo kukarabati kiwanja hicho ambacho kikikamilika kitatoa fursa nyingi za kiuchumi.

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango, alisema anampongeza Rais Dk. John Magufuli, kwa kupeleka fedha za ukarabati wa kiwanja hicho.

Habari Kubwa