Ukatili unaojiri dhidi ya watoto wanaobadili petroli kuwa bangi

19Dec 2021
Elizaberth Zaya
Dar es Salam
Nipashe Jumapili
Ukatili unaojiri dhidi ya watoto wanaobadili petroli kuwa bangi
  • Ni sura nyingine ya ukatili dhidi ya kundi hilo

​​​​​​​NI majira ya saa 12 asubuhi, jua likiashiria mawio, watoto wenye umri wa kuwa shule ya msingi, wanaonekana wakipita katikati ya magari yaliyosimama eneo la Ubungo Mataa mkoani Dar es Salaam, wakiomba msaada kwa abiria wa daladala.

Watoto wakitumia chupa iliyowekwa petroli ambayo huitumia kwa kunusa kupata ulevi.

Kwa Dar es Salam kukutana na watoto wa umri huo wakiomba msaada barabarani ni jambo la kawaida kwa wenyeji wa mkoa huo wa kibishara, lakini kinachoshuhudiwa Ubungo safari hii huenda kikawa kigeni kwa wengi.

Kwa nini? Macho ya watoto hao yanaonekana kama ya mtu aliyelewa, hata namna wanavyotembea, ni ishara tosha kwamba kuna kilevi wametumia. Macho yao yamelegea mithili ya mlevi wa pombe au mtumiaji wa dawa za kulevya.

Si hivyo tu, midomo ya baadhi yao inaonekana kuwa na unyevunyevu unaofanana na mate na pua zao zinaonekana kuzidiwa na wingi wa kamasi.

Kingine ambacho Nipashe Jumapili inakibaini na kupatwa na maswali yanaisukuma kufanya udadisi, ni watoto hao kuvaa sweta lenye mikono mirefu ilhali hali ya hewa Dar es Salaam kipindi hiki ni ya joto kali.

Pembeni ya barabara ya Nelson Mandela, jirani na makutano ya barabara nne eneo la Ubungo, anaonekana mmoja wa watoto hao akinunua vitumbua na chai kwa mfanyabishara mdogo wa chakula na hapo ndipo Nipashe inapata nafasi ya kupata undani wa madhila yanayowakabili watoto hao.

"Nina miezi mitatu sasa tangu nianze kufanya kazi hii ya kuomba. Ninaishi hapa kwa sababu ndugu yangu ninayemtegemea, ambaye alinitoa kwetu Mbeya kuja hapa Dar (es Salaam) alikamatwa na polisi," anasimulia mtoto aliyejitambulisha kwa jina la Jafari.

Mtoto huyo (9) anaendelea na simulizi yake, akitamka: "Kaka yangu ndiye alikuwa ananilea, alinitoa Mbeya, lakini alikamatwa na kupelekwa polisi, nikabaki napata shida ndiyo nikawa natembea kila sehemu kuomba chakula hadi nikafika hapa Ubungo.

"Hapa kuna wenzagu (watoto) wengine wengi. “Sijui kama nitampata kaka yangu na sikumbuki tulikokuwa tunaishi, naishi kwa shida sana hapa, mpaka niombe pesa kwa watu ndiyo ninunue chakula na nisipopata nalala njaa.

"Sehemu ya kulala yenyewe ni ya shida, tunaruka uzio uliowekwa chini ya daraja la juu ndio tunalala humo. Humo tunamolala askari wanatufukuza, huwa tunajificha sana."

Mtoto huyo anadai kuwa katika eneo hilo la Ubungo, kuna watoto zaidi ya 50 ambao wanaishi maisha hayo ya kuomba na wengi wao wametoka mikoa mbalimbali kwa kuletwa na ndugu zao kisha kutelekezwa.

Katika udadisi wake kupitia ushuhuda wa mtoto huyo, Nipashe Jumapili inabaini watoto wengi walio katika eneo hilo, wameshajiingiza kwenye uvutaji kilevi wanachokitengeneza kwa kuchanganya mafuta ya petroli na gundi inayotumika kwenye viatu.

"Ukiwaona watoto wengi hapa utaona wako kama mateja, wanavuta gundi wanaiweka kwenye chupa ya plastiki halafu wanaificha kwenye sweta mkononi, halafu wanavuta, ila mimi sivuti.

"Sivuti kwa sababu wanaovuta wanalegea na wanasinzia tu ovyo, wanasema hiyo inawasaidia kuwaondolea aibu wanapoomba kwenye gari na wengine wakilewa hivyo wanalala mchana ili usiku ndiyo waanze kuomba na wasilale kwa sababu wanaogopa kubakwa na yale mabaunsa 'yanayotukimbizaga' usiku.

"Kuna wenzetu (watoto) wamekubali yaishe, wame... (alitamka neno lenye dhana ya kufanyiwa ukatili), wanatembea kama wana ulemavu, utawaona tu wapo wengi hapa," anasema mtoto huyo.

Wakati mazungumzo na Jaffari yakiendelea, linatokea kundi la wenzake 10 baadhi yao wakiwa wameshika chupa za plastiki zikiwa zimechomekwa mirija ndani, huku wakitamka maneno yaliyokosa tafsida, wakitaka huduma ya chakula kwa 'mama ntilie'.

Mmoja wa watoto hao, Kizito (jina la pili tunalihifadhi) anasema wamejifunza kuvuta kilevi hicho baada ya kupata darasa kutoka kwa mwenzao na wanaona kinawasaidia kupata usingizi na kuwaondolea aibu katika kazi yao hiyo ya kuomba.

"Yaani ukipiga hii dada yangu (mwandishi), dunia unaiona raha sana na unapiga kazi balaa, hakuna cha aibu wala kumwogopa mtu. Hata wewe ukijaribu utaipenda na hutatamani kuacha," adai Kizito huku akisogeza chupa yenye kilevi hicho kwenye mdomo wa mwandishi.

Kizito anabainisha wananunua gundi Manzese na mafuta ya petroli huyanunua kwenye vituo vya mafuta, akifafanua uzoefu wao kwamba lita moja inatumika kwa kundi lao la Ubungo kwa siku mbili, kila mmoja akichangia ununuzi huo.

“Petroli tunanunua sheli kwenye kichupa cha maji ya kunywa (anaonyesha chupa), tunajichangisha pesa, lakini gundi huwa tunapata kwa mtu mmoja eneo la Manzese, anajulikana sana kwa jina la bibi. Kichupa kidogo kama hiki cha juisi (anaonyesha) anatuuzia Sh. 1,000," alisema.

USHUHUDA MAMA NTILIE

Peter Lucas, fundi viatu eneo la Ubungo, anasema kumekuwa na ongezeko la idadi ya watoto kwenye eneo hilo na wanapowahoji, wanadai wametelekezwa na watu waliowatoa mikoani kuwaleta Dar es Salaam.

"Niko hapa muda mrefu sasa nikifanya kazi hii ya kushona viatu. Kila siku sasa idadi ya watoto inaongezeka, matokeo yake vitu wanavyofanya na kufanyiwa hapa ni vya hatari.

"Wengine kama unavyoona ni watoto wadogo lakini wameshakuwa mateja kwa kuvuta hiyo gundi wanayochanganya na petroli, kwenye hizo chupa zao ndimo wanamoweka, tumekuwa tukiwanyang`anya ukiwaona wanavuta ndiyo maana unaona wanaficha, lakini hawasikii.

"Kibaya zaidi wakishalewa hivyo, wakienda kuomba kule kwa wenye magari yao, watu wazima wengine wasio na hofu ya Mungu wanawabeba kwenye magari yao kuondoka nao na wakirudi hapa unaona wanachechemea tu. Ukimuuliza anakwambia kaharibiwa.

"Na hivi karibuni kuna watoto kama watatu hivi tuliwaonea huruma tukawapeleka hapo Hospitali ya Sinza Palestina, walikuwa wameharibika wanapepesuka, wanajidondokea tu," alisema.

Fundi Lucas anaishauri serikali kuwasaidia watoto hao kwa kuwaondoa katika eneo hilo ili wasiharibu watoto wengine.

Mama ntilie katika eneo hilo, Mariam Hamis, anasema anapata wakati mgumu kuwauzia chakula watoto hao kwa kuwa wanakuwa wamelewa kiasi cha baadhi yao kutokwa na udenda mdomoni, hivyo anaingiwa hofu ya kupoteza wateja wake.

“Unakuta mtoto anakuja hapa amechafuka, anapepesuka na anatoa udenda mdomoni na ameshika hizo dawa wanazovuta mkononi. Kwa hiyo mpaka unaona ukimpatia chakula kwenye sahani wanazotumia wateja wengine wa kawaida unaona utawapoteza.

"Nimelazimika kutafuta vyombo maalumu kwa ajili yao tu, na wateja wangu wanalijua hilo. Lakini mimi ni mama, huwa nawaonea huruma, nawapatia chakula na kipimo chao huwa ni tofauti, huwa wananunua cha Sh. 1,000 badala ya Sh. 1,500 .

"Wakati mwingine anakuja hapa anakwambia hana pesa na ana njaa, umkopeshe, inabidi umpe tu, akipata analeta na ni waaminifu sana. Inabidi serikali iwaondoe, la sivyo watazidi kuvuta wengine na kuwaharibu zaidi," Mariam anashauri.

Katika ufuatiliaji wake, Nipashe Jumapili pia ilibaini watoto wengine waliotumbukia kwenye matumizi ya kilevi hicho wako kwenye Kituo cha Mabasi cha Magufuli.

Bibi anayeuza gundi inayotumiwa na watoto hao (jina tunalo), anaiambia Nipashe Jumapili eneo la Manzese kuwa ana wateja wengi na huwa hafuatilii wala kuwahoji matumizi yake kwa wateja wake.

Daktari wa Binadamu katika Hospitali ya Sinza Palestina, Dk. Gloria Lema, anayetoa huduma kwenye kitengo maalumu kinachoshughulikia watoto waliofanyiwa ukatili na walioathirika na dawa za kulevya, anakiri wamekuwa wakipokea watoto waliothiriwa na dawa za kulevya.

"Tumepokea baadhi ya watoto ambao wanavuta kilevi wanachochanganya petroli na gundi. Baada ya kupokea wengi wa namna hii ilibidi tufuatilie na ndipo tukabaini kwamba wanalazimika kutumia kilevi hiki baada ya serikali kufanya kazi ya ziada ya kudhibiti dawa hizi zingine za kulevya, kwa hiyo wengi wamegeukia kwenye aina hiyo ya ulevi.

“Gundi na petroli ni kilevi kingine kibaya kama ilivyo kwa bangi au dawa zingine za kulevya na zinaathiri mambo mengi mwilini ikiwamo afya ya akili na ndiyo maana mtu anayetumia aina hii lazima muda wote anaishiwa nguvu na anakuwa anasinzia. Akizoea kutumia lazima awe na uraibu na kupona kwake akiamua kuacha inachukua muda mrefu kidogo," Dk. Gloria anasema.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Judith Kimaro, anasema wana taarifa ya watoto hao na wamekuwa wakiwasaidia kuwapeleka kwenye vituo vya kusaidia walioathiriwa na dawa za kulevya.

Pili Missana, mmiliki wa kituo cha kusaidia walioathirika na dawa za kulevya kilichoko Kigamboni, Dar es Salaam, anasema kwa mwezi amekuwa akipokea wastani wa watoto 10 wanaovuta gundi iliyochanganywa na petroli na kuwakabidhi kwa maofisa ustawi wa jamii.

KAMISHNA KUSAYA

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya, anasema gundi, petroli, shisha havijajumuishwa katika Sheria Na. 5 ya Mwaka 2015 ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.

"Mimi mwenyewe nimekutana na hao watoto wanaovuta hiyo gundi, na siyo siri wameharibika, lakini kwa bahati mbaya sheria inayotuongoza haijajumuisha hivyo vitu, la sivyo wadau wakae tena na kujadili kupeleka sheria bungeni ili ifanyiwe marekebisho," anasema.

Anasema watoto wanaovuta dawa za kulevya nchini wapo na baadhi yao wako kwenye vituo ambavyo vimetengwa na serikali kwa ajili ya kuwapatia dawa waathirika wa dawa hizo.

"Na kuna mmoja nilimkuta kwenye kituo chetu mkoani Tanga, ana miaka 16 na nilipozungumza naye anashindwa hata kuongea vizuri, anasema alianza kutumia dawa tangu akiwa darasa la tano, na tunapokea taarifa pia kutoka shule mbalimbali za sekondari na msingi kuhusiana na watoto wanaovuta dawa hizo," anasema.

Kusaya anabainisha kuwa takwimu walizonazo kwa sasa zinaonyesha zaidi ya watu 500,000 nchi nzima wanatumia dawa za kulevya na wengi wao wakiwa ni vijana wenye umri wa kuanzia miaka 16 hadi 45.

Haki za watoto zinalindwa katika mikataba mikubwa miwili ya kimataifa ukiwamo wa Haki za Mtoto (CRC) wa mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa mwaka 1990, yote ikiwa imeridhiwa na Tanzania.

Vilevile, Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inaelekeza wajibu wa serikali, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwalinda watoto.

Habari Kubwa