'Ukatili wa kijinsia bado tishio nchini'

07Mar 2020
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
'Ukatili wa kijinsia bado tishio nchini'

KANSELA Mkuu wa Ushirikiano na Maendeleo wa Serikali ya Canada kupitia ubalozi wake nchini, Gwen Walmsley, amekutana na wadau kutoka mashirika 39 ya kiraia yanayojishughulisha na masuala ya haki za binadamu kupokea matokeo ya stadi ya awali ya ukatili wa kijinsia katika mikoa ya Kilimanjaro na...

Mmoja wa wawezeshaji wa mradi wa kukuza usawa kwa kutumia elimu ya haki za binadamu, unaotekelezwa na Shirika la Tusonge kwa ufadhili wa taasisi ya kimataifa ya Equitas, Daudi Massawe, akitoa mrejesho kuhusu stadi ya awali ya ukatili wa kijinsia, katika mkutano wa wadau wa mashirika ya kiraia kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, uliofanyika katika Manispaa ya Moshi, jana. PICHA: GODFREY MUSHI

Arusha.

Walmsley alikwenda mkoani Kilimanjaro jana kuzindua awamu ya pili ya mradi wa kukuza usawa wa kijinsia kwa kutumia elimu ya haki za binadamu.

Mradi huo wa miaka mitano umekuwa ukitekelezwa nchini tangu mwaka 2019 na Shirika la Tusonge CDO kwa ufadhili wa Serikali ya Canada kupitia uhusiano wa kimataifa na wabia wa Taasisi ya Equitas.

Katika Mkoa wa Kilimanjaro, mradi huo unatekeletezwa kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Wilaya ya Siha, wakati mkoani Arusha, unatekelezwa Jiji la Arusha na Wilaya ya Meru.

Kansela Walmsley alipewa taarifa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tusonge, Agnatha Rutazaa, licha ya jitihada nyingi zilizofanyika kulinda haki za msingi za binadamu, bado hakuna usawa hasa kwa wanawake na wasichana.

“Kwa hali ya sasa, ukatili wa kingono umekithiri kwa wanawake na watoto, wanawake hawaruhusiwi katika kufanya uamuzi wa kipato cha familia na mara nyingi kinamama wanaachwa nyuma katika kufanya uamuzi wa matumizi ya mapato ya familia na wasichana hawapewi fursa ya elimu.

“Kansela Mkuu wa Ushirikiano na Maendeleo katika Ubalozi wa Canada ambao ndiyo wanafadhili mradi huu, amekuja kutuunga mkono na kushirikiana pamoja nasi.

"Lengo kubwa la kufika hapa Moshi ni kufanya uzinduzi wa mradi rasmi na kuangalia kipengele kikubwa cha kurejesha matokeo ya stadi ya awali yaliyofanyika Oktoba mwaka 2019. Stadi hiyo imefanyiwa uchambuzi na matokeo yake yatangazwa Machi mwaka huu," alisema.

Kwa mujibu wa Rutazaa, wadau hao watapata fursa ya kutoa maoni yao kama kuna mawazo au maoni ya mambo ambayo yalionekana yako kwenye jamii, lakini hayakujitokeza wakati wa upimaji na tathmini.

“Tunarejesha matokeo hayo ya stadi ya awali kwa wadau muhimu wa haki za binadamu katika Mkoa wa Kilimanjaro na mradi utatumia mbinu shirikishi katika kukuza usawa wa kijinsia ikijumuisha kujenga uelewa na uwezo, kushirikiana katika kampeni za uhamasishaji, mipango tekelezi ya jamii na majukwaa," alisema.

Lengo la baadaye la mradi huo ni kuwapo kwa ongezeko la uwezo wa wanawake na watoto wa kike katika kukuza usawa wa kijinsia ndani ya jamii.

Habari Kubwa