Ukawa wapata upenyo Zanzibar

09Dec 2016
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Ukawa wapata upenyo Zanzibar

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ni kama sasa umepata upenyo kufanya mikutano yake baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusema vyama vya siasa vinaweza kufanya kampeni kwenye uchaguzi wa madiwani katika kata 22 Tanzania Bara na ubunge katika Jimbo la Dimani, Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) -Zanzibar, Salum Mwalimu.

Hii ni baada ya kupita miezi sita tangu Rais John Magufuli apige marufuku mikutano ya kisiasa hadi mwaka 2020.
Uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Dimani unatarajia kufanyika Januari 23, mwakani.

Juni 24, mwaka huu, Rais Magufuli aliwataka Watanzania na wanasiasa kuachana na siasa hadi ifikapo wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020, akiwataka kujikita katika kufanya kazi.

Rais Magufuli alieleza kuwa siasa zinazopaswa kufanywa, ni zile za wawakilishi waliochaguliwa na wananchi ambao wanapaswa kuzifanya katika mabaraza ya madiwani na bungeni pekee. wanapowawakilisha wananchi.

Akizungumza na Nipashe lililotaka kufahamu kama kampeni za uchaguzi wa madiwani na ubunge zinazotarajiwa kuanza Desemba 23, mwaka huu zitaruhusiwa, Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, vyama vya siasa vinaruhusiwa kufanya kampeni katika maeneo yao husika.

Kailima alisema kampeni za uchaguzi zinaweza kufanywa na mgombea husika, chama chake ama wakala wake atakayemteua hivyo kampeni zinaruhusiwa kufanyika katika maeneo husika tu na siyo nje ya majimbo.

Alipoulizwa endapo viongozi wa juu wa vyama husika wataruhusiwa kusafiri kwenda kufanya kampeni katika kata 22 na Jimbo la Dimani Zanzibar, Kailima alisema Nec haisimamii kampeni za uchaguzi bali inaratibu shughuli za uchaguzi.

“Kufanya kampeni ni haki yao kisheria, kampeni zinaweza kufanywa na mgombea mwenyewe ama chama chake au wakala atakayemteua kufanya kampeni kwa ajili yake, lakini msininukuu kuwa NEC imeruhusu mikutano ya vyama vya siasa,” alisema Kailima.

CHADEMA WANASEMAJE
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) -Zanzibar, Salum Mwalimu, alisema kuruhusiwa kufanyika kwa kampeni, ni jambo la kisheria na ni haki ya vyama kufanya kampeni.

Alisema Chadema itafanya kampeni kama ilivyo kawaida kwa chaguzi nyingine na viongozi mbalimbali watakuwapo katika uchaguzi huo wa Jimbo la Dimani Zanzibar.

Alisema Ukawa visiwani Zanzibar waliwakilishwa na Chama cha Wananchi (CUF) katika jimbo hilo.

Mwalimu alisema ugomvi baina ya CUF Zanzibar ni kati yao na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na siyo NEC, hivyo uchaguzi huo Ukawa watashiriki kwa nguvu moja.

“Tutashiriki katika kufanya kampeni na tutashiriki katika uchaguzi, baadhi ya viongozi watakuwapo ila siwezi kujua nani na nani watakuwapo,” alisema Mwalimu.

KAULI YA CCM
Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema wao wamejipanga kushinda kwenye uchaguzi huo wa madiwani na ubunge kwa nguvu zote.

Alisema CCM itapeleka timu ya kampeni katika jimbo husika kulingana na nguvu inayostahili.

Ole Sendeka alifafanua kuwa CCM itashiriki katika uchaguzi huo kama ilivyoshiriki chaguzi zilizopita, lakini bado haijafahamika ni viongozi gani watakaokwenda kufanya kampeni.

“Idara inayohusika na uchaguzi imejiandaa, CCM ngazi ya wilaya, kata wote wapo tayari kwa kufanya kampeni, hivyo ni imani yangu kuwa tutashinda uchaguzi huo,” alisema Ole Sendeka.

Uchaguzi wa marudio wa ubunge Jimbo la Dimani, utafanyika baada ya kutokea kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ally Tahir, huku uchaguzi wa madiwani katika kata 22 utafanyika baada ya kuongezwa kwa wilaya mbalimbali.