Ukawa washindwa msimamo wao

22Jun 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Ukawa washindwa msimamo wao

KATIKA kile ambacho ni kinyume cha msimamo wa wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutembea juu ya kauli yao, jana waliingia ndani ya ukumbi wa Bunge huku wakisalimiana na waenzao wa CCM.

Mbunge wa sumve (ccm), Richard Ndassa akimsalimia mbunge wa iringa (chadema),peter msigwa huku mbunge wa ubungo (chadema) saed kubenea akimziba mdomo ili asimjibu.

Wabunge hao, juzi walitoka kwa staili mpya ya kufunga midomo kwa karatasi na plasta na kuahidi kutosalimiana, kushirikiana, kuingia bungeni na kukaa kwenye mgahawa wa Bunge na wabunge wa CCM hadi bunge litakapoahirishwa Julai Mosi, mwaka huu.
Wabunge hao wako kwenye mgomo dhidi ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, kwa madai ya kutoridhishwa na uendeshaji wa Bunge.

Wanadai Naibu Spika anaendesha bunge kwa ubabe na kubaka demokrasia, hivyo kuahidi kutoingia kwenye kikao au eneo ambalo atakuwepo hadi atakapokubali kujirekebisha.

Jana ilikuwa siku ya 22 kwa wabunge hao kususia vikao vya Bunge tangu kuanza kwa mjadala wa Bajeti ya mwaka 2016/17, ambapo hawajawahi kuingia zaidi ya kuwasilisha taarifa mbalimbali, ikiwamo hotuba ya upinzani ya bajeti mbadala na msomaji alipotakiwa kumtambua Naibu Spika alikataa kufanya hivyo hadi alipolazimisha na kudai kuwa anahitaji uheshimiwa na kuanzia sasa wao wataitana ndugu.

Hata hivyo, nje ya ukumbi wa Bunge, Nipashe ilishuhudia Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), akiwa ameshikana mikono na Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola.

Hata hivyo, wakati wa asubuhi ndani ya ukumbi, Msigwa alikatazwa kupokea salamu ya Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, kumziba mdomo kwa karatasi.

Hali hiyo pia ilijitokeza kwa Lugola alipotaka kumsalimia na kujitahidi kumsemesha Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Magereli, lakini hakutaka kuitikia salamu hiyo wala kumsemesha.

Wabunge wa Ukawa juzi katika kikao chao, waliazimia kutoshirikiana na wabunge wa CCM wala kusalimiana na kutopeana mikono.
Pamoja na hayo, pia wamejitoa kwenye makundi yote ya mitandao ya kijamii ikiwamo ‘Whatsapp’, ambayo walikuwa pamoja na wabunge wa CCM na hata kantini ya Bunge hawataingia na hawatashiriki mkichezo pamoja.

Habari Kubwa