Ukiendesha gari umelewa kutupwa 'selo' hadi mwakani

18Dec 2020
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Ukiendesha gari umelewa kutupwa 'selo' hadi mwakani

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta, ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani mwake kuwakamata madereva walevi na kuwaweka lupango hadi sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya zitakapopita. Lengo la kiongozi huyo ni kupunguza ajali na kulinda uhai wa wananchi.

Alitoa agizo hilo wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yaliyoadhimishwa Viwanja vya Ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha na Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa huo (TPF NET).

Alisema kumekuwa kujitokeza ajali zisizo za lazima kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka, zinazosababishwa na madereva wazembe wasiotaka kufuata sheria za nchi kwa kunywa pombe kupita kiasi kisha kuendesha vyombo vya moto.

"Sasa hapa mkoani kwangu sitaki ajali za makusudi kuanzia sasa, RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) ninakuagia, ukikuta mtu amelewa huku anaendesha chombo cha usafiri, kamata weka ndani mpaka sikukuu zote hizi zipite, ninajua wataongea sana sababu dhamana ya haki ni ya kila mmoja, lakini uhai wa kila mtu ni mali ya serikali, hivyo lazima tuulinde kwa kukuhifadhi ndani," aliagiza Kimanta.

Alisema kumekuwa na tabia ya watu kukamatwa na kuwekwa lupango kisha baada ya siku moja au siku hiyo hiyo, wanapewa dhamana, akisisitiza "tabia hiyo ikome".

Kimanta alisema madhara yanayosababishwa na madereva walevi ni makubwa kuliko wao kusaidiwa kuhifadhiwa ndani.

Aliwaomba wananchi kuchukua tahadhali ya kutoacha nyumba zao bila watu katika kipindi hiki kuelekea sikukuu hizo mbili.

"Hivi sasa wahalifu wamebadili mfumo, wanavunja nyumba mchana na kuiba badala ya usiku kwa sababu ya doria za polisi zinatisha, sasa nanyi wananchi hakikisheni mnaweka watu nyumbani, msitoke wote, japo polisi wataongeza doria mchana na usiku ila nanyi chukueni tahadhali," alishauri.

Kimanta alisema ingawa Jeshi la Polisi limejitahidi kulinda maeneo yote, kila mtu anapaswa asimame katika nafasi yake na kufichua wahalifu anaowafahamu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salumu Hamduni, alisema amepokea maelekezo ya mkuu huyo na atayafanyia kazi, ili kila mmoja aheshimu sheria za barabarani na sikukuu zipite kwa usalama bila ajali mkoani humo.

Habari Kubwa