Ukombozi afya waja kwa maelfu

11Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Accacia
Nipashe
Ukombozi afya waja kwa maelfu

WAKAZI zaidi ya 2,598 wa kijiji cha Nyankolongo Kata ya Nundu, Tarafa ya Bukwimba, wilayani Nyang’hwale mkoani Geita, wanatarajia kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wakitafuta huduma ya afya baada ya kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu mgodi wa Accacia kutoa vifaa vya ujenzi wa.....

zahanati ya kijiji hicho.

Kuja kwa ukombozi huo kulibainishwa jana na Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Nyang’olongo, Masumbuko Robert, alipokuwa akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa zahanati hiyo kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Hamim Gwiyama, wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo.

Ofisa huyo alisema kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 2,598 kati yao wanawake 1,339 na wanaume 1,239, kinachangamoto kubwa ya ukosefu wa huduma ya afya, ambapo wananchi hulazimika kutembea umbali mrefu wa kilometa kumi kwenda kutafuta huduma hiyo kwenye zahanati ya kata ya jirani ya Bukwimba na umbali wa kilometa zaidi ya 20 kufika Hospitali ya Wilaya Kharumwa.

Kwamba changamoto hiyo imekuwa ikichangia vifo vya wajawazito na watoto kutokana na wengine kushindwa kumudu gharama za usafiri na hivyo kwenda kwa waganga wa tiba asilia.

Robert alibainisha kuwa kufuatia changamoto hiyo ya muda mrefu, Mei mwaka jana, waliamua kuanza ujenzi wa jengo la zahanati ya kijiji hicho, ili kukabiliana na vifo vya wajawazito na watoto ambalo lifikia hatua ya kupaua baada ya wananchi kukubaliana kuchangia Shilingi 60,000 kila mmoja, ambapo wakazi 502 wenye uwezo wa kufanya kazi wamechangia Shilingi 22,080,000 kwenye ujenzi huo.

Sarah Shija Mabula, mkazi wa kijiji hicho, alisema ukosefu wa huduma ya afya ni changamoto kubwa kwa wakazi wa kijiji hicho, hususani wajawazito hali hiyo huwalazimu kutembea zaidi ya kilometa 20 kwenda Hospitali ya Wilaya Kharumwa na wengine hujifungulia majumbani na kupoteza maisha kutokana na kutokwa damu nyingi wakati wakijifungua, hivyo kuiomba serikali kusaidia haraka ujenzi huo huku akiipongeza Acacia kwa hatua hiyo.

Diwani wa Nundu, Juma Petro, alisema wananchi wa kata hiyo wamehamasika kuchangia wenyewe ujenzi wa zahanati ili kukabiliana na adhaa ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya na kwamba kata hiyo ina vijiji vitatu Nundu, Igeka na Nyang’olongo, ambavyo vimekamilisha ujenzi wa maboma ya zahanati na utakapokamilika utapunguza vifo vya wajawazito na watoto.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Acacia Bulyanhulu na Buzwagi, Benedictor Busunzu, akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Hamim Gwiyama, alisema vifaa vya ujenzi wa zahanati, mabati, mbao vyote kwa pamoja vina thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 62.

Busunzu alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati kumi kwenye vijiji vya halmashauri hiyo, kufuatia makubaliano ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 32 kwenye vijiji vya wilaya hiyo, huku akiahidi kuendelea kusaidia kwenye miradi ya maendeleo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Hamim Gwiyama, aliwataka maofisa watendaji wa kata na vijiji pamoja na wenyeviti wa vijiji na vitongoji wilayani humo kusimamia zahanati hizo kwa uadilifu, huku akisisitiza vifaa hivyo vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Mariam Chaurembo, alisema kuwa serikali inaendelea na mkakati wake wa ujenzi wa zahanati kila kijiji kama sera ya serikali inavyoelekeza.