Ukusanyaji mbovu takwimu wamkera Dk. Shein

08Jan 2017
Mwinyi Sadallah
Nipashe Jumapili
Ukusanyaji mbovu takwimu wamkera Dk. Shein

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema bado kuna tatizo la ukusanyaji, utumiaji na uhifadhi wa takwimu Zanzibar, hivyo kutaka kuwapo mfumo mmoja madhubuti wa utekelezaji wa suala hilo.

Dk. Shein alisema hayo jana, baada ya kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Ofisi za Mtakwimu Mkuu wa Serikali, zinazojengwa Mazizini, Wilaya ya Mjini Unguja, ambazo zitagharimu Sh. bilioni 7.9. uzinduzi huo ulifanyika ikiwa sehemu ya shamrashamra za Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Udhaifu katika utoaji wa takwimu na taarifa ni ukiukaji wa maadili ya uongozi na utumishi wa umma,”alisema Rais Dk. Sheini na kuagiza kila wizara kuwa na mtaalamu wa takwimu katika Idara ya Mipango na Sera ili kuimarisha utoaji wa takwimu za uhakika.

Alieleza taarifa sahihi haziwezi kupatikana bila ya kuwa na mfumo mzuri wa kitaalamu wa ukusanyaji wa takwimu, huku akisisitiza kuwapa wananchi habari na taarifa sahihi za serikali ni haki yao ya kikatiba na halina budi kutekelezwa na viongozi na watendaji wakuu wa serikali.

“Mimi mwenyewe ni mtumiaji mkubwa wa takwimu, lakini unapohitaji takwimu kutoka wizarani basi kwa wakati mmoja tarajia kupata takwimu tofauti,” alisema Dk. Shein.

Pia alisema kuna haja ya kuondokana na utaratibu uliopo sasa wa kila mmoja kuwa na mamlaka ya kutoa takwimu za serikali na kutaka kuwe na utaratibu maalumu.

Dk. Shein alitaka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu takwimu na umuhimu wake katika mipango ya maendeleo.

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania, Dk. Ashatu Kijaji, alisema ujenzi wa jengo kama hilo unafanyika mjini Dodoma chini ya ufadhiliwa wa Benki ya Dunia.

Dk. Kijaji alitumia nafasi hiyo kumwomba Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kuendelea kuzisaidia taasisi za takwimu ili kukamilisha miradi yote miwili na kusisitiza kuwa takwimu zina umuhimu mkubwa katika kufanikisha dira ya maendeleo ya 2025 Tanzania na 2020 ya Zanzibar.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Elizabeth Ann Talbert, alisema takwimu zina umuhimu katika kupanga mipango ya maendeleo na Benki ya Dunia itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha takwimu.

Habari Kubwa