Ukuta Mirerani kujengwa miezi 6

14Nov 2017
Sanula Athanas
Nipashe
Ukuta Mirerani kujengwa miezi 6

SERIKALI imesema ujenzi wa ukuta kuzunguka eneo la mgodi wa tanzanite Mirerani mkoani Manyara ulianza rasmi Jumatatu ya wiki iliyopita na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti (kulia) akikagua maandalizi ya ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani.

Ujenzi huo unafanyika kutokana na agizo la Rais John Magufuli la Septemba 20 alipotembelea eneo hilo na kutoa amri kujengwe haraka ukuta kuzunguka maeneo yote ya machimbo ya tanzanite.

Akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2018/19 na Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti ya mwaka ujao wa fedha, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, alisema tayari ujenzi wa ukuta huo umeanza ukifanywa na wanajeshi zaidi ya 2,000.

Alisema tayari serikali imeshatoa asilimia 80 ya fedha zinazohitajika kukamilisha mradi huo.

Ilikadiriwa kuwa ujenzi huo ungegharimu Sh. bilioni 4.8, kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutokana na ziara ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi mapema mwezi huu.

"Ujenzi huo umeanza toka Novemba 6 na ujenzi huu unakwenda kwa kasi ya hali ya juu," Nyongo alisema, "Jeshi letu la JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) liko 'site' (eneo la ujenzi) linafanya kazi ya 'construction' (ujenzi).

"Na kwa hali iliyopo 'site', kuna wanajeshi wametoka JKT zaidi ya 2,000 wanafanya kazi hiyo na wataifanya kazi hiyo kwa mkataba unavyosema, watafanya kazi ndani ya miezi sita na fedha za ujenzi wa ukuta huo wamekwishapewa fedha asilimia 80."

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa ukuta huo kutadhibiti utoroshaji wa madini kutoka eneo la Mirerani.

'Vilevile Mheshimiwa Rais alitoa amri kwamba tujenge mnada, tutengeneze mnada ambao utakuwa Mirerani ambao utatumika kwa watu wanaokuja kununua madini ya tanzanite," alisema.

"Na hapa tunapozungumza, pale Mirerani tumeshakwisha kupata eneo la EPZ A ambalo Sh. bilioni 2.2 imetolewa kwa ajili ya ujenzi wa haraka wa mnada ule na ukishakamilika ujenzi ule kwa muda mfupi ujao, basi mnada ule utafunguliwa, madini ya tanzanite, maonyesho ya madini, wanunuzi watakuja pale, watanunua na watalipa mrabaha, watalipa ili tuweze kupata kipato chetu kama tunavyostahili."

Alisema serikali sasa ina wataalamu wazuri wa uthaminishaji wa madini ambao tayari wamefanikisha kukamatwa kwa dhahabu na almasi ya mabilioni ya shilingi ikiwa mbioni kupelekwa ughaibuni.

"Mfano mzuri ni juzi juzi tu kuna hawa WDL (Williamson Diamond Limited), waliweza kuzalisha almasi, almasi ile katika kutolewa kuisafirisha, serikali kwa juhudi zake ilikamata na kuangalia kulinganisha uthaminishwaji wa mwanzo na na wa pili, tukakuta thamani ya almasi ile ni kubwa," alisema.

Nyongo aliongeza: "Tumekamata dhahabu Zanzibar yenye thamani ya Sh. milioni 500. Tunaendelea kuimarisha ulinzi mipakani kuhakikisha kwamba utoroshaji wa dhahabu unasimamishwa, lakini wakati huo huo serikali ina juhudi ya kuanzisha minada mitano mikubwa ambayo itakuwa inauza dhahabu.

"Tutauza dhahabu kwa njia ya wazi, watu waje kununua dhahabu na waweze kulipa ushuru, waweze kulipa mrabaha. Lakini vilevile minada yetu hii tunatakiwa tuitengenezee miundombinu mizuri kwa maana ya usalama, umeme, maji, na ya usafirishaji."

Naibu Waziri huyo pia alimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake kuhakikisha analinda rasilimali ya nchi.

Alisema mchango wa rasilimali ya madini hapo nyuma ilikuwa asilimia 3.7, lakini sasa sekta hiyo inachangia asilimia 4.3 katika uchumi wa nchi."

Habari Kubwa