Ukuta waua wanafunzi Dar

07Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ukuta waua wanafunzi Dar

WANAFUNZI wawili wameripotiwa kufariki dunia jijini Dar es Salaam, huku wengine wakijeruhiwa kutokana na kuangukiwa na ukuta wa shule.

WAKAZI WA ENEO HILO WAKISHUHUDIA UKUTA HUO ULIOANGUKA NA KUSABABISHA VIFO VYA WANAFUNZI HAO.

Waliofariki dunia ni Sabra Salum (8) wa darasa la pili na Nasri Mjenge (7) wa darasa la kwanza, wote wa Shule ya Msingi Bwawani iliyoko Mtoni Kijichi.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Evelyn Nasri, tukio hilo lilitokea jana majira ya asubuhi wakati wanafunzi hao wakipita karibu na ukuta huo.

“Waliojeruhiwa ni watatu, lakini mimi ninamtambua mmoja wa shuleni kwangu ambaye ni Sharifa Jumanne (9) wa darasa la tatu, wawili wametibiwa katika Hospitali ya Temeke na mwingine Mbagala na kuruhusiwa,” alisema.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kuanguka kwa ukuta huo na kusababisha vifo vya wanafunzi wawili.

“Ni kweli kuna ukuta umeanguka na kusababisha vifo vya wanafunzi wawili, huo ukuta ulikuwa umechakaa, hivyo kupitisha maji mara kwa mara,” alisema Kamanda Mambosasa.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula, alisema wakati wa tukio hilo kulikuwa na wanafunzi watano waliokuwa wamekaa eneo moja.

Kamanda Lukula alisema ukuta ulipowaangukia wasamaria wema waliwachukua na kuwawahisha hospitali, lakini kabla ya kufika hospitalini wawili walishafariki dunia.

“Hali za hawa watatu ambao wamelazwa katika Hospitali ya Temeke hali zao ni nzuri na tunatarajia wanaweza kuruhusiwa kama hali zao hazitabadilika,” alisema Kamanda Lukula.

Habari Kubwa