Ulinzi mkali kesi ya Mbowe Kisutu

07Dec 2018
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ulinzi mkali kesi ya Mbowe Kisutu

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, jana walifikishwa katika Mahakama ya Kisutu chini ya ulinzi mkali.

Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (wa pili kushoto), Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji (kushoto), Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika (kulia) na Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa wakiwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kesi inayowakabili ya uchochezi kutajwa na kuahirishwa hadi Desemba 21 mwaka huu. PICHA: GETRUDE MPEZYA

Wakati vigogo hao wa Chadema wakifikishwa mahakamani hapo, mahakama imemruhusu Mbunge wa Kawe, Halima Mdee,  kwenda Burundi kwenye michezo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Jana, kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri, aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.

 

Saa 2: 28 asubuhi msafara wa washtakiwa mbalimbali wakiwamo Mbowe, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, na washtakiwa wengine, uliingia katika viunga vya mahakama hiyo ukiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza na Polisi.

 

Kadhalika, mahakama hiyo ilizingirwa na ulinzi mkali wa askari kanzu na wale wenye sare za majeshi hayo, huku kikosi maalum cha mbwa kikizunguka katika viunga hivyo pamoja na wanahabari wa vyombo mbalimbali nchini.

 

Saa 3:30 Mbowe na Matiko waliongozwa nchini ya ulinzi mkali wa zaidi ya askari 10 kuingia katika ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo, huku wafuasi na washtakiwa wengine wakisalimiana nao baada ya kufikishwa ukumbini humo kutoka mahabusu.

 

Hatimaye kesi hiyo ilitajwa na upande wa Jamhuri ukiongozwa na jopo la Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Dk. Zainabu Mango na Wakili wa Serikali Wankyo Simon, ulidai kuwa kesi imepangwa kwa ajili ya kutajwa lakini washtakiwa wawili hawapo mahakamani.

 

Wakili wa utetezi Peter Kibatala alidai kuwa washtakiwa saba kati ya tisa wapo mahakamani, Mdee kupitia Katibu Mkuu wa Bunge, amewasilisha barua kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu akiomba kuhudhuria michezo ya mabunge.

 

Kwa upande wa Heche, tarehe iliyopita aliwasilisha vielelezo na barua kwamba mke wake amepata upasuaji wa uzazi na kwamba bado hali za mama na mtoto hazijaimarika.

 

Nchimbi alidai kuwa washtakiwa wote wawili wamefuata taratibu za kisheria, Jamhuri haina pingamizi na maombi yao.

 

Hakimu Mashauri alisema kweli mahakama yake imepokea barua ya kuomba ruhusa Mdee na Heche imekubali maombi hayo mpaka Desemba 21, mwaka huu washtakiwa wote wafike mahakamani kusikiliza kesi yao.

 

Mbali na Mbowe, Matiko, Mdee, Heche wengine ni, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, wa Bunda, Ester Bulaya na katibu Mkuu Taifa, Dk. Vincent Mashinji.

 

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.

 

Katika hatua nyingine,  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetoa ruhusa kwa Mbunge wa Kawe, Mdee, kuhudhuria michezo ya Mabunge ya Afrika Mashariki nchini Burundi.

 

Hatua hiyo imetokana na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha barua ya kumwombea ruhusa mpaka Desemba 20, mwaka huu.

 

Mbali na Mdee, mahakama hiyo imetoa ruhusa kwa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, anayeuguliwa na mke na mtoto wake. Wabunge hao na vigogo wengine saba, akiwamo Mwenyekiti Taifa wa Chama vha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, wanakabiliwa na mashtaka 13 ya uchochezi.

Habari Kubwa