Ulinzi mkali kisa Lowassa

28Jun 2017
Gwamaka Alipipi
Dar es salaam
Nipashe
Ulinzi mkali kisa Lowassa

HALI ya ulinzi katika barabara za katikati ya jiji, eneo la Posta Dar es Salaam, jana uliimarishwa vikali na Jeshi la Polisi wakati Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, akihojiwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI).

Magari ya polisi yanayorusha maji ya kuwasha, 'difenda' yenye askari pamoja na askari kanzu, walionekana wakiranda randa katika maeneo hayo tangu majira ya saa nne asubuhi.

Lowassa alikuwa akihojiwa na Jeshi la Polisi kutokana na matamshi aliyoyatoa Juni 24 usiku wakati wa futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara.

Kwenye mwaliko huo, Lowassa alimtaka Rais John Magufuli kutafakari upya hatima ya masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki) maarufu kama Uamsho, walio mahabusu kwa zaidi ya miaka minne wakikabiliwa na kesi ya ugaidi.

Lowassa alinukuliwa zaidi akieleza kuwa ni jambo la fedheha kwa nchi iliyopata uhuru zaidi ya miaka 50 kuwaweka mahabusu viongozi wa dini bila kesi kusikilizwa mahakamani.

Tangu kuwasili kwa Lowassa katika Makao Mkuu ya Jeshi la Polisi, majira ya saa nne asubuhi, ulinzi ulikuwa mkali katika barabara zote zinazoingia katika jengo la makao makuu ya Jeshi hilo.

Katika maingiliano ya Barabara ya Ohio na Ghana Avenue, kulikuwa na gari la polisi lenye kutumia maji ya kuwasha likiwa limeegeshwa kufunga njia na gari kama hilo pia lilionekana limeegeshwa katika makutano ya Ghana Avenue na Barabara ya Azikiwe, karibu na jengo la Posta mpya. Lango kuu la Makao Makuu ya Polisi lipo Ghana Avenue.

Mbali na ulinzi huo, askari waliovalia kiraia walionekana wakirandaranda mitaa ya Posta mpya, baadhi wakiwa na radio za mawasiliano ya masafa mafupi.
Kadhalika, gari la Polisi aina la Land cruiser likiwa na askari kadhaa lilifanya doria kuzunguka mitaani.

Hadi Lowassa anamaliza kuhojiwa majira ya saa 8:05 mchana na kuondoka katika makao makuu ya Polisi, ulinzi ulikuwa bado mkali.

Habari Kubwa