Ulinzi waimarishwa kisa kudhibiti viboko

07Aug 2019
Gurian Adolf
KATAVI
Nipashe
Ulinzi waimarishwa kisa kudhibiti viboko

ASKARI wa wanyamapori wa Pori la Akiba la Rukwati mkoani Katavi, wamewasili katika kijiji cha Shanwe Manispaa ya Mpanda kwa ajili ya kuweka ulinzi katika bwawa la Milala lililovamiwa na viboko zaidi ya 60.

VIBOKO.

Askari hao wamepelekwa ili kuimarisha usalama wa wananchi wa kijiji hicho kutokana na hatari zinazotokana na viboko hao.

Meneja wa pori hilo, Pachwi Mlwina, alisema uamuzi huo umetokana na athari ambazo wananchi hao wamekuwa wakizipata kutokana na kuwapo kwa viboko hao kwani hali inazidi kuwa mbaya kutokana na kuwajeruhi na kuwaua.

Alisema  kwa muda mrefu wananchi hao wamekuwa wakiomba serikali  kuwavuna viboko hao kwa kuwa wamekuwa kero kwao kutokana na kula mazao yao, kuwanyima uhuru kutokana na kuingia mpaka kijijini na kuwadhuru.

Meneja huyo alisema kutokana na hali hiyo, uongozi wa pori hilo la akiba umeamua kuweka kambi maalumu ya askari wake ambao wataimarisha ulinzi ili kuwalinda wananchi hao kwa kuwa hawawezi kuvumilia kuona watu wakiendelea kupoteza maisha wakati uwezo wa kuwalinda wanao.

Alisema askari hao watakuwa wakiishi katika kijiji hicho mpaka hapo itakapokuwa vinginevyo, lengo ni kuhakikisha wananchi wanaendelea na maisha bila kuathirika.

Katibu Tawala wa mkoa huo, Abdala Malela, aliwaeleza wananchi hao kuwa serikali imesikia kilio chao cha muda mrefu, hivyo wasiwe na wasiwasi kwa kuwa watapewa ulinzi na wataendelea na shughuli zao.

Hata hivyo, aliwataka kuacha tabia ya kuwachokoza wanyamapori kwani kijiji chao kipo karibu na pori la akiba la Rukwati.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Saloma Kaliki, aliishukuru serikali kwa kusikia kilio chao, na kuwaomba askari wa wanyamapori wawahakikishie ulinzi wame wanapokwenda kuvua samaki katika bwawa hilo kwa sababu wanalitegemea kwa ajili ya kupata kitoweo.

Ulinzi huo umewekwa zikiwa ni siku chache baada ya watu wawili kuuawa na wanyama hao walipokuwa wamekwenda katika bwawa hilo kuvua samaki kwaajili ya kitoweo.