Umaskini Tanzania wapungua,Wanufaika Tasaf marufuku kuchagia maendeleo

17Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Umaskini Tanzania wapungua,Wanufaika Tasaf marufuku kuchagia maendeleo

Mkurugenzi  Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt Albina Chuwa ameeleza kuwa takwimu za hali ya umaskini wa kipato hapa nchini kwa mwaka 2017, zimepungua kwa kiasi kikubwa na kufikia asilimia 26 na kwamba jukumu la kuondoa umaskini kwa mtu mmoja mmoja ni jukumu la watu wote.

Mkurugenzi  Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt Albina Chuwa.

Hayo ameyabainishwa leo Februari 17, 2020 mbele ya Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Tasaf jijini Dar es Salaam.

"Hali ya umaskini wa kipato hapa nchini Mwaka 1991-92 ulikuwa Asilimia 39, 2007 umaskini ulikuwa asilimia 34, 2012 Asilimia 28.4 na 2018 hali ya umaskini likuwa 26.4, kasi ya kupungua umaskini hapa nchini inaenda kwa mwendo wa kasi" amesema Dkt Albina Chuwa Mkurugenzi wa Takwimu.

Aidha akitoa takwimu za umaskini kwa nchi zingine za Afrika Dkt Chuwa amesema,"Rwanda utafiti wao wa mwisho ulikuwa Mwaka 2015, na hali ya umaskini ilikuwa Asilimia 38.2, Kenya 2015 ni asilimia 36.3, Afrika Kusini Asilimia 55.5, Zambia Asilimia 54.4,na kwa mwaka huo huo Zimbabwe ilikuwa ni Asilimia 72.3, hii ndiyo hali ya umaskini ya mahitaji ya msingi kwa Nchi za Afrika".

Hayo yamejiri katika uzinduzi wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF, mpango ambao utazinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Katika uzinduzi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika amesema haiwezekani wanufaika wa TASAF wakatwe fedha za maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule za Sekondari wakati wenye uwezo wa kufanya hivyo hawajatoa michango hiyo.

Mkuchika amesema ilishatokea kwenye baadhi ya maeneo, akibainisha kuwa Serikali za mitaa ziliwakata fedha wanufaika hao. Amesema aliagiza fedha hizo kurudishwa lakini jambo hilo halijafanyika, “katika baadhi ya mamlaka za Serikali za mitaa wakiwa na michango ya Sekondari, hela rahisi kuipata ya Tasaf wanaenda kuikata.

Niliagiza zile halmashauri warudishe hela zao.” “Michango ya maendeleo wanapaswa kuchanga watu wenye uwezo, hawezi mtu amepewa 20,000 akapambane na umaskini anakatwa mchango wa Sekondari wakati aliye na uwezo hakatwi hata shilingi moja.”

 

Habari Kubwa