Umeya Dar sasa kaa la moto

11Jan 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Umeya Dar sasa kaa la moto

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi madogo ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, kuweka zuio la kuondolewa kwenye nafasi yake.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, picha mtandao

Imeelezwa na mahakama hiyo kuwa sababu za kutupilia mbali maombi hayo ni kutowasilishwa uthibitisho wa kufanyika kikao cha kumwondoa madarakani wala hasara atakayoipata atakapoondolewa katika wadhifa huo.

Lakini, mahakama hiyo imekubali ombi la kwanza la kuongezwa muda wa kujibu hati kinzani ya walalamikiwa, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Uamuzi huo ulisomwa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega, aliyesikiliza maombi hayo madogo.

Alisema kuwa baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili, mahakama imeona kwamba mlalamikaji ameshinda ombi lake la kwanza la kutaka kuongezwa muda wa kuwasilisha majibu ya hati kinzani.

Alisema ili mahakama isikilize kesi ya madai, ni lazima nyaraka zote muhimu zikamilike dhidi ya maombi ya msingi kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu ombi la pili la mlalamikaji, mahakama imeona kwamba Wakili wake, Hakima Mwasipo, alikuwa na wajibu wa kuthibitisha uwapo wa kikao cha kumwondoa Mwita madarakani.

Alisema ni lazima mahakama ipewe maelezo juu ya uwapo wa kikao cha kumwondoa katika nafasi yake ya umeya ili ifikie uamuzi wa kutoa haki.

"Kwa kuwa mlalamikaji ameshindwa kuithibitishia mahakama hii kuhusu kikao cha kumwondoa kwenye nafasi yake ya umeya,
inatupilia mbali hoja za kutaka abaki madarakani kwa sababu hoja zake kupitia wakili wake hazina miguu ya kusimamia kwa kushindwa kufuata vigezo ikiwamo kueleza kuhusu kufanyika kikao cha kutaka kumtoa madarakani," Hakimu Mtega alisema.

Alisema ili maombi yabaki katika nafasi yake, inatakiwa kuwapo kwa zuio la awali kuwezesha kitu hicho kubaki katika nafasi yake na kisiondoshwe.

Alisema mahakama hiyo ina maoni kwamba wakili wa mwombaji alikuwa na wajibu wa kuthibitisha uwapo wa kikao cha kumwondoa madarakani Mwita.

Akizungumzia hoja ya kesi kutajwa, Hakimu Mtega alisema kesi hiyo ilikuja Januari 8, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na si kusikilizwa kwa kuwa bado mawakili walikuwa katika hatua ya kubadilishana nyaraka.

Alisema wakili wa wajibu maombi ambaye ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata, alipotoka kwa kutaka mahakama iendelee na usikilizwaji wakati kesi hiyo imekuja kwa kutajwa.

Alisisitiza kuwa ni lazima mahakama ihakiki taratibu zote za usikilizaji wa shauri zinafuatwa kwa mawakili kubadilishana nyaraka ambazo ni hati ya kiapo, hati ya kiapo kinzani na majibu ya hati ya kiapo kinzani ndipo kesi ianze kusikilizwa.

Hata hivyo, alisema maombi ya msingi yenye usajili namba 3/2020, yatasikilizwa Januari 13, mwaka huu.

Katika madai ya msingi, Mwita anapinga mchakato wa kuondolewa kwenye nafasi yake ya umeya, akidai umekiuka utaratibu.

Meya huyo anadaiwa kupendelea madiwani wa chama chake katika uundaji wa kamati mbalimbali bila kumshirikisha Mkurugenzi wa Jiji, kutumia mali (gari) za ofisi vibaya na kushindwa kufanya matumizi ya hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Habari Kubwa