Ummy aionya NEMC kufanya kazi kipolisi

13Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ummy aionya NEMC kufanya kazi kipolisi

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu, amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuacha kufanya kazi kama polisi badala yake lishirikiane na wawekezaji.

Pia amelitaka baraza hilo kukaa na wawekezaji na kuwasaidia katika azma yao ya ujenzi wa viwanda badala ya kuwa kikwazo katika kutekeleza azma hiyo ya serikali.

Ummy alisema hayo juzi alipotembelea kiwanda cha BTY cha kurejeleza betri za magari kwa ajili ya kupata malighafi za kutengeneza betri na bidhaa zingine za plastiki, Buguruni jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Ummy aliambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey, na uongozi wa NEMC ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Esnath Chaggu na Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Dk. Samuel Gwamaka.

Waziri Ummy alisema mwekezaji hakuandaa mpango wa usimamizi wa ardhi kulingana na bidhaa anazozitengeneza kama vile utiririshaji wa majitaka, vumbi wakati wa uzalishaji hali inayopelekea uchafuzi wa mazingira.

Kutokana na hali hiyo, Ummy aliagiza NEMC kukaa na mwekezaji kuangalia ni namna ya kuepuka madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira na kwamba uwekezaji uende sambamba na kuhakikisha Sheria ya Mazingira inafuatwa ili kulinda afya za wananchi na mazingira kwa ujumla.

Soma zaidi: https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa