Ummy amuahidi makubwa JPM

23May 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Ummy amuahidi makubwa JPM

WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amemuahidi, Rais John Magufuli kuwa ataendelea kuitumikia nchi kwa bidii, uaminifu na maarifa zaidi.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku moja tangu Rais Magufuli kumwagia sifa waziri huyo kuwa katika janga la virusi vya corona, amejituma na kuchapa kazi licha ya kwamba hana taaluma ya udaktari.

Juzi, wakati Rais Magufuli akiapisha viongozi mbalimbali aliowateua, alisema Waziri Ummy alisimamia wizara hiyo kwa ujasiri mkubwa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Waziri Ummy aliandika: ‘Asante Rais Magufuli kwa kuendelea kuniamini na kunitia moyo katika kusimamia sekta ya afya nchini hasa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya corona’.

“Naahidi kuendelea kuitumikia nchi yangu kwa bidii, uaminifu na maarifa zaidi.”

Rais Magufuli alisema Waziri Ummy anajituma katika suala hilo la corona na amesimama licha ya kwamba hana taaluma ya udaktari.

“Kuna wakati fulani niliona anasimama peke yake kwenye wizara, yeye siyo daktari wa kusomea, unajiuliza mwanasiasa anasimama peke yake kuzungumzia taaluma ya udaktari, wasaidizi wake wote ni madaktari huoni matokeo, nakupongeza sana Ummy najua nilikutesa.

“Sitaki kueleza mengi, lakini ni kweli aliteseka kwa sababu kwa siku mara nyingine alikuwa anapigiwa simu zaidi ya mara nane iwe saa nane iwe saa ngapi, unapokuwa kwenye vita saa nyingine kubembelezana hapana.”

Habari Kubwa