Ummy ataja vipaumbele 13 afya 2022/23

17May 2022
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ummy ataja vipaumbele 13 afya 2022/23

WIZARA ya Afya imetenga Sh. trilioni 1.1 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele 13 ili kuboresha huduma za afya ikiwamo ujenzi wa hospitali maalumu ya mama na mtoto utakaogharimu Sh. bilioni 10.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Akiwasilisha jana bungeni Dodoma, Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema kati ya fedha hizo za matumizi ya kawaida ni Sh. bilioni 554.3 na miradi ya maendeleo ni Sh. bilioni 555.13.

Ummy alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuimarisha utoaji wa huduma za chanjo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na kusimamia viwango vya ubora wa huduma za kinga na tiba katika ngazi zote za utoaji huduma za afya nchini.

“Tutawapima watoa huduma wetu katika hospitali zetu kuangalia ubora wa huduma, tutaangalia kwanza mgonjwa alivyofika katika kituo cha huduma alipata huduma nzuri ikiwamo kuchukuliwa historia yake, vipimo na dawa zote.

“Tutaangalia lugha na muda ambao mgonjwa ametumia katika kupata huduma za afya, tutasimamia ubora wa huduma za afya,” alisema.

Alitaja eneo lingine kuwa ni kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga pamoja na mimba za utotoni.

“Tunakwenda kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa na vitendanishi katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya na kuimarisha huduma za lishe hususani kwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano, vijana balehe na wanawake wa umri wa kuzaa,” alisema.

Vipaumbele vingine, kwa mujibu wa Waziri Ummy, ni kuimarisha huduma za afya na usafi wa mazingira ili kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini na kuimarisha miundombinu yake ikiwamo katika Hospitali za Rufani za Mikoa, Kanda, Maalum na Taifa.

Alitaja vipaumbele vingine ni kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi, kudhibiti magonjwa ya mlipuko, magonjwa ya kuambukiza na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kuimarisha utoaji wa mafunzo ya wataalamu katika sekta ya afya na kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini.

“Kuimarisha utawala bora na uwajibikaji katika utoaji huduma za afya na kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na matumizi ya takwimu katika utoaji wa huduma za afya nchini.

Alisema wanataka pamoja na kujivunia majengo ya hospitali, vituo vya afya na zahanati waanze kusimamia namna huduma za afya zinavyotolewa kuanzia mgonjwa anavyoingia hospitalini mpaka anapopata huduma.

Waziri Ummy alisema ili kutekeleza vipaumbele hivyo, katika mwaka 2022/23, wizara imekadiria kutumia Sh. trilioni 1.1 kutekeleza majukumu ya wizara ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa ofisi na miradi ya maendeleo.

Alitaja baadhi ya miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha kwa mwaka 2022/23 ni kununua, kutunza, kusambaza na kutoa chanjo kwa watoto nchini ambapo kiasi cha Sh. bilioni 74. 4 zimetengwa.

Sh. bilioni 23.36, alisema  zimetengwa kwa ajili ya kujenga vyumba vya huduma za watoto wachanga katika hospitali 100 za wilaya, kuwajengea uwezo watoa huduma kuwa na stadi, weledi na tabia bora katika kutoa huduma za mama na mtoto, kujenga, kuweka vifaa na watumishi wenye weledi kwenye ICU za wazazi katika hospitali za kanda na mikoa.

Alisema miradi mingine ni kuwezesha ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi na kuzisambaza katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya ambapo kiasi cha Sh. bilioni 200 zimetengwa na kukamilisha ujenzi wa hospitali tano za Rufani za Mikoa katika mikoa mipya ya Katavi, Geita, Njombe, Songwe na Simiyu ambapo jumla ya Sh. bilioni 18.6 zimetengwa.

Miradi mingine ni kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya tatu za rufani za mikoa katika mikoa ya Shinyanga, Singida na Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mara ambapo Sh. bilioni 26 zimetengwa na kuboresha huduma za matibabu ya ubingwa bobezi katika Hospitali ya Taifa na Kanda.

Alisema fedha hizo zitatumika kuimarisha miundombinu na ununuzi wa vifaa katika Taasisi ya JKCI, Hospitali za Rufani za Kanda za Chato, Mtwara, KCMC, Bugando, Mbeya na kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Magharibi.

“Kuimarisha Hospitali Teule ya Ukerewe ambapo Sh. bilioni 16.9 zimetengwa na kuendelea na ujenzi wa wodi ya wagonjwa binafsi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Sh. bilioni 4 zimetengwa,”alisema.

Miradi mingine itakayotekelezwa mwaka 2022/23 alisema ni kuanza ujenzi wa jengo la kutolea huduma za uchunguzi na tiba ya saratani ikiwamo huduma ya mionzi katika Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dodoma, Sh. bilioni 10 zimetengwa na kuendelea kukamilisha upanuzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika hospitali nane za rufani.

 Hospitali hizo za rufani zitajengwa katika mikoa ambayo mikataba yake bado inaendelea ambazo ni Ligula (Mtwara), Tumbi (Pwani), Bombo (Tanga), Kagera, Maweni (Kigoma), Kitete (Tabora), Sekou – Toure (Mwanza) na Mawenzi (Kilimanjaro) ambapo kiasi cha Sh. bilioni 13.7 kimetengwa.

Kadhalika alisema wataendelea na ujenzi wa hospitali mbili mpya za mikoa ya Ruvuma na Sokoine (Lindi) ambapo Sh. bilioni 2 zimetengwa.

Habari Kubwa