Undani kutimuliwa Simba, Madabida

15Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Undani kutimuliwa Simba, Madabida
  • *Kinana afichua kile walichomfanyia Magufuli

HATIMAYE Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kueleza kiundani kile kilichowaponza baadhi ya makada wake waliotimuliwa mwishoni mwa wiki wakiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba na Mwenyekiti wake katika Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida.

Akizungumza kwenye kikao cha UWT mjini Dodoma jana, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye alimtuma mwakilishi, alisema wale waliotimuliwa baada ya kuvuliwa uanachama Jumamosi (Machi 11), walikutwa na makosa kadhaa yanayohusiana na maadili ikiwamo kuendelea kubaki kwenye makundi ya watu waliokuwa wakiwaunga mkono wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya chama chao hata baada ya kuteuliwa kwa Rais John Magufuli kupeperusha bendera yao.

Kinana ambaye katika mkutano huo wa UWT alikuwa akiwakilishwa na Katibu wa zamani wa NEC Idara ya Oganaizesheni ya CCM, Dk. Muhammed Seif Khatib, alisema kitendo hicho cha kutomuunga mkono Magufuli, ni baadhi ya makosa yaliyowaponza wahusika hadi wakavuliwa uanachama na kwamba hiyo ni ajali ya kisiasa kwa wahusika.

Wakati wa kuelekea chaguzi mbalimbali, kila mwana-CCM hutakiwa kuachana na kambi ya watu waliokuwa wakiwaunga mkono na kushirikiana kuhakikisha kuwa wagombea waliopitishwa kwenye vikao vyao halali ndiyo wanaungwa mkono ili mwishowe wafanye vizuri dhidi ya wapinzani.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Kinana (kupitia Dk. Khatib), makada waliotimuliwa hawakuonekana kuwa tayari kumuunga mkono Magufuli aliyekuwa ameshateuliwa na CCM bali kung’ang’ania kambi za watu wao, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni na taratibu za CCM na hivyo wakaadhibiwa na Kamati ya Maadili na Usalama ya chama hicho.

Mbali na Simba na Madabida, vigogo wengine wa CCM waliovuliwa uanachama ni aliyekuwa mwenyekiti wao katika mkoa wa Mara, Christopher Sanya; Jesca Msambatavangu aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Iringa na pia Erasto Kwilasa aliyekuwa akishikilia cheo hicho katika mkoa wa Shinyanga.

Wakati akitangaza adhabu dhidi ya makada mbalimbali wa chama chao, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, aliwataja watuhumiwa wengine wa makosa ya kimaadili na hatua zilizochukuliwa dhidi yao kuwa ni pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Brazili, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliyeamuriwa kuiomba radhi CCM kutokea hukohuko ughaibuni na Adam Kimbisa aliyesamehewa makosa yake.

Hivi sasa, Kimbisa ni Mbunge wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM katika Mkoa wa Dodoma na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC).

Wengine waliochukuliwa hatua mbalimbali ni pamoja na baadhi ya wenyeviti wa CCM wa wilaya na wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

Wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM mwaka 2015, Simba, Kimbisa na Nchimbi walikuwa ni miongoni mwa vigogo wa CCM waliojitokeza hadharani kupinga uamuzi wa chama chao kumuengua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa miongoni mwa wagombea.

John Magufuli ndiye aliyeibuka mshindi katika kinyang’anyiro hicho kabla ya kutwaa urais baadaye kwa kupata asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa, akimshinda Lowassa aliyechepukia upinzani na kugombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

ONYO LA KINANA
Akiendelea kuzungumza kwenye kikao hicho cha UWT alichomuwakilisha Kinana, Khatib alisema watu waliokumbana na adhabu ya kufukuzwa uanachama wamepata ajali ya kisiasa ambayo kwa kawaida huwa haiangalii kama mhusika ni mwanaume au mwanamke; au kama ni mkubwa au mdogo.

Alisisitiza umuhimu wa kina mama na wanachama wengine CCM kuhakikisha kuwa wanafuata maadili ili wajiepushe na ‘ajali’ za aina hiyo.

Aidha, Khatib alitumia nafasi hiyo ya kumuwakilisha Kinana kujitolea mfano yeye, akisema kuwa amekitumikia chama kwa muda mrefu na kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka huu na pia amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu kwa takriban miaka 20.

Seif ni miongoni mwa viongozi watatu waliopumzishwa katika uongozi CCM ambapo sasa nafasi yake inashikiliwa na Pereira Ame Silima.

Viongozi wengine wapya ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa NEC, Dk. Frank Haule na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdallah Juma Abdallah.
 
MSAMBATAVANGU, MADABIDA
Katika hatua nyingine, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Dar es Salaam, Madabida na Mwenyeki wa CCM Mkoa wa Iringa,
Msambatavangu, wameeleza kwa nyakati tofauti kuwa hawawezi kueleza lolote kuhusiana na misimamo yao kwa sasa hadi hapo watakapopata barua rasmi za kuwavua uanchama wao ndani ya CCM.

Akizungumza na Nipashe jana, Msambatavangu alisema bado hajakabidhiwa rasmi barua ya kufukuzwa uanachama na kwamba yupo tayari kwa ajili ya kuipokea wakati wowote.

“Nimeshasema bado sijakabidhiwa barua ya kufukuzwa uanachama na hivyo siwezi kuzungumza jambo lolote kwa sasa,” alisema.
Aidha, Madabida alisema vilevile kuwa hawezi kuzungumzia jambo lolote kwa sasa na kwamba, anasubiri kupata barua.

“Siwezi kuzungumza chochote sasa … naomba unielewe, siwezi kuzungumza kitu chochote,” alisema Madabida na kuagana na mwandishi.

Wengine waliokumbwa na adhabu hizo hawakupatikana ili kueleza misimamo yao. Hata hivyo, Sophia Simba alikaririwa jana akisema kuwa amekubali na atabaki kuwa mkereketwa wa CCM na kwamba, kamwe hafikirii kuhamia chama kingine cha siasa.

*Imeandikwa na Augusta Njoji (Dodoma) na Mary Geofrey (Dar).

Habari Kubwa