UNIDO yaahidi mema kwa sekta binafsi

09Mar 2018
Romana Mallya
Nipashe
UNIDO yaahidi mema kwa sekta binafsi

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), limeahidi ushirikiano kwa sekta binafsi ili nchi iweze kufikia ndoto yake ya uchumi wa viwanda na utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Li Yong (wa pili kushoto), akiwa mwenye furaha na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi (kushoto), Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage (katikati), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Dk. Samuel Nyatahe, wakati wa hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na CTI kwa ajili yake, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: JOHN BADI

Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, Li Yong, alitoa ahadi hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, viongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) wafanyabiashara na wenye viwanda nchini.

Yong ambaye yupo nchini kwa mwaliko wa Waziri Mahiga, alisisitiza kuwa sekta binafsi ni muhimu kwa maendeleo na kwamba lazima uwepo ushirikiano kati ya Serikali na sekta hiyo ili kuifanikisha.

Akitoa salamu za shukrani, Mwenyekiti wa CTI Dk. Samwel Nyantahe, ndiye aliyesema Yong yupo nchini kwa mwaliko wa Waziri Mahiga na kwamba hiyo ni mara ya nne kuja Tanzania.

Akizungumza zaidi katika hafla hiyo, Yong alisema UNIDO itaisaidia Tanzania ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030 hasa lengo la tisa na la 17.

Lengo la tisa la SDG linazungumzia kuunganisha na kujenga miondombinu ya kudumu ili kukuza viwanda vilivyoendelea wakati lengo la 17 likisisitiza ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii.

“Tunaunga mkono nchi kufikia malengo endelevu ya kupunguza umaskini... TPSF pia inafanya kazi kwa kushirikiana na serikali kutekeleza mpango wa maendeleo ya miaka mitano ya nchi,” alisema.

Yong alisema sekta binafsi inachangia zaidi ya asilimia 18 ya utoaji wa ajira ulimwenguni.

Alisema sekta hiyo imetoa mchango mkubwa katika kukuza elimu na upelekaji bidhaa nje ya nchi.

Alisema UNIDO mbali ya kuangalia serikali inavyofanya kazi na sekta binafsi, pia huangalia malengo ya Tanzania katika kuwainua wananchi na kuondoa umaskini.

Waziri Mwijage alisema Tanzania na UNIDO walisaini makubaliano ya ushirikiano siku chache zilizopita kwa sababu shirika hilo limeisaidia China kufika ilipo sasa.

Mahiga alisisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo yenye uwezo wa kuchangia ukuaji wa maendeleo ya uchumi hivyo kuna haja UNIDO kuipa nguvu ili kutimiza malengo hayo.

Mwenyekiti wa TPSF, Dk. Reginald Mengi, alisema  wachumi wengi, hususan wale wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, wameonyesha kuwapo kwa ukuaji wa uchumi katika miaka ya hivi karibuni lakini kukuwa huko hakuendani na utajiri wa nchi husika.

Aidha, Dk. Mengi alisema sekta binafsi na jumuiya ya wafanyabiashara wametoa mchango mkubwa katika ukuaji wa viwanda.

“UNIDO watashirikiana na serikali na sekta binafsi katika kuinua uendelezaji wa viwanda, tunaweza kuchukulia mfano wa baadhi ya maeneo kama sehemu ya kuanzia na baadaye tukaangalia maeneo mengineyo kwa ujumla,” alisema.

Dk. Mengi alisema wanatambua mchango wa UNIDO katika kusaidia sekta binafsi kwa maendeleo ya Tanzania.

Habari Kubwa