Ununuzi mitambo ya kisasa waboresha maabara za mkemia mkuu

13Jan 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Ununuzi mitambo ya kisasa waboresha maabara za mkemia mkuu

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imenunua mitambo tisa yenye thamani ya Sh. bilioni 6.5 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa mamlaka hiyo.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko. picha mary geofrey

Aidha, kutokana na kuwapo kwa mitambo hiyo ya kisasa, wamepunguza siku za kupima vinasaba na kutoa majibu kutoka ndani ya siku 21 hadi siku moja kwa sasa.

Mafanikio hayo yalielezwa leo jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, wakati akizungumza na waandishi wa habari na maofisa mawasiliano wa taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, walipotembelea mamalaka hiyo.

"Uwekezaji huu wa mitambo ya kisasa, umeongeza kasi na uwezo wa GCLA kufanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali zikiwamo za dawa za kulevya, uchunguzi wa mazingira, vinasaba vya binadamu na wanyama na ubora wa chakula,"amesema Dk. Mafumiko.

Amesema kuwapo kwa mitambo hiyo ya kisasa pia kumesaidia kutoa huduma kwa wingi na kwa kasi kulinganisha na miaka ya nyuma. Aidha, amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kukarabati miundombinu ya ofisi za kanda zote nchini kwa gharama ya Sh. bilioni 1.3, uliosaidia kuboresha utendaji kazi.

Dk. Mafumiko amesema katika kipindi hicho pia walifanikiwa kusajili wadau wa kemikali 2,426, kusajili vibali 21,336 na kutoa vibali 99,934 pamoja na kufanya kazi katika mipaka yote na katika bandari nchini kwa saa 24.

Habari Kubwa