Unyanyapaa unachangia maambukizo mapya VVU'

24Mar 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Unyanyapaa unachangia maambukizo mapya VVU'

KUENDELEA kwa unyanyapaa katika jamii dhidi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), kunachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa maambukizo mapya visiwani Zanzibar.

Ofisa Habari, Mawasiliano na Uhamasishaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC), Sihaba Saadat Haji, aliyasema hayo katika kikao kazi na waandishi wa habari kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Studio Rahaleo.

Alisema wapo baadhi ya watu wanashindwa kujitokeza kuzungumzia hali zao kwa kuhofia kunyanyapaliwa katika maeneo yanayowazunguka hasa kwenye familia na sehemu za kazi.

Alisema hali ya unyanyapaa kwa Zanzibar ni zaidi ya asilimia 23.4 na kwamba maeneo ya vijijini upo juu zaidi kulinganisha na maeneo ya mjini hasa kisiwani Pemba ambao upo kwa asilimia 38.

Ofisa Saadat alisema mikoa inayoongoza kwa unyanyapaa huo ni Kaskazini Pemba asilimia 45.4, Kusini Pemba asilimia 32.4, Kaskazini Unguja asilimia 29.4, Kusini Unguja 19.3 na Mjini Magharibi asilimia 16.6.

Alisema unyanyapaa unatokea katika sehemu mbalimbali, lakini maeneo yanayoongoza kwa unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU ni maeneo ya kazi, tiba na ibada.

Akizungumzia athari za unyanyapaa katika jamii, ofisa huyo alizitaja kuwa ni pamoja na mzazi, kujenga hofu ya kupima, hivyo hupelekea kuongezeka kwa maambukizo mapya, mtoto kukosa huduma stahiki kutokana na hofu ya mzazi kujulikana na jamii, watoto hudumaa na kukosa kukua vizuri kimwili na kiakili, kukosa fursa ya kucheza na kuchanganyika na wenzao na baadaye hufariki dunia.

Ofisa huyo alisema kuna umuhimu mkubwa wa kupunguza hali ya unyanyapaa ili kupunguza kasi ya kuenea kwa VVU, watu watajitokeza kupima afya zao, kurahisisha uwazi na mmoja kumweleza mwenza wake hali yake ya maambukizo, kuondoa tatizo la kuvunjika kwa ndoa kusiko kwa lazima na kupunguza vifo vinavyotokana na Ukimwi.

Sambamba na hayo, alisema bado elimu inahitajika zaidi kwa jamii kuacha kuwanyanyapaa watu wanaoishi na VVU ili kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa huo kwa kupunguza maambukizio mapya.

Mratibu kutoka Mradi wa Afya Kamilifu (AMREF), Sandey Bebwa, alisema kwa kushirikiana na ZAC, wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuondoa unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU na kuleta mabadiliko ndani ya jamii.

Alisema vikwazo vilivyopo ni uwelewa mdogo kwa jamii kuhusu unyanyapaa, hivyo wataendelea kuchukua hatua zinazofaa ikiwamo kuendelea kuelimisha jamii ili kuondokana na dhana hiyo potofu.

Akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Kulinda na Kusimamia Mambo ya Ukimwi ya Mwaka 2013, Mwanasheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira, Saada Said, alisema sheria hiyo imekataza kumpima mtu kwa lazima bila ya hiari yake isipokuwa tu kama kuna amri ya mahakama, mjamzimto, mtu anayechangia damu na aliyebakwa ama mbakaji.

Habari Kubwa