Upatikanaji vifaa tiba kwa wenye ualbino kupatikana mikoa tisa

26May 2020
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Upatikanaji vifaa tiba kwa wenye ualbino kupatikana mikoa tisa

CHAMA cha watu wenye ualbino (TAS), mkoa wa Morogoro, kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine wamefanikiwa kuimarisha upatikanaji wa tiba ya awali ya saratani ya ngozi kwenye mikoa tisa ya Tanzania Bara pamoja na Unguja Zanzibar.

Baadhi ya viongozi Wa TAS wakionesha vifaa tiba vitakavyoanza kutolewa kwa watu wenye ualbino mkoani Morogoro (picha na Christina Haule, Morogoro)

Mwenyekiti wa TAS mkoa wa Morogoro, Hassan Mikazi, alisema hayo kwenye taarifa aliyoitoa kwa waandishi wa habari na kuwa lengo ni kufanikisha kuwepo kwa vifaa tiba hivyo kwenye mikoa yote Tanzania ili kuwawezesha watu wote wenye ualbino na wasio na Ualbino kupata huduma hiyo wakiwa kwenye maeneo yao kwa wakati wakianza na mikoa hiyo.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni pamoja na mkoa wa Morogoro, Lindi, Mara, Singida, Iringa, Tanga, Dodoma, Dar es Salaam na Unguja-Zanzibar.

Aidha, Mikazi amesema, vifaa tiba hivyo vya saratani ya ngozi awali vilizinduliwa rasmi tarehe 13 Juni 2019, katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro na kupelekwa kwenye hospitali za Mikoa hiyo saba iliyotajwa nchini.

Amesema Chama hicho kimefanikiwa kufanya ushawishi kwa serikali kuanza kununua mafuta kinga ya ngozi (Sunsreen lotions) kupitia taasisi ya saratani ya Ocean Road na baadhi ya halmashauri za wilaya nchini.

Hata hivyo, amesema kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kuongeza uelewa kuhusu ualbino sambamba na kuadhimisha miaka 40 tangu kusajiliwa kwa TAS hapa Tanzania, wataendesha kliniki ya ngozi sambamba na tiba ya ubaridi mkali kwa watakaopatikana na viashiria vya saratani ya ngozi katika mikoa hiyo.

Amesema kutokana na janga la Corona wameshindwa kuandaa maadhimisho hayo katika upana zaidi kama ilivyokuwa zamani na watawaita wahusika kufika kwenye kliniki hizo kupata tiba hizo.

Mikazi amesema kliniki hizo zitatoa tiba na dawa kwa nyakati tofauti kila mkoa na kwa Mkoa wa Morogoro itafanyika tarehe 27- 28 Mei 2020 na kilele kitafanyika tarehe 13 Juni mkoani hapa.

Habari Kubwa