Upepo wa JPM kutikisa kaskazini

18Oct 2020
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Upepo wa JPM kutikisa kaskazini

MGOMBEA Urais, Dk. John Magufuli (JPM), anatarajia kuendelea na kampeni ya duru la mwisho katika Mkoa ya Pwani kisha kuhamishia makali katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Dodoma.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole, aliyasema hayo jana jijiji Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali.

Polepole alisema kuwa Oktoba 19, mwaka huu, Dk. Magufuli ataanza kufanya kampeni za awamu ya mwisho katika Mkoa wa Pwani na baadaye atatikisa mikoa ya kaskazini mwa nchi.

“Siku ya terehe 19 (kesho), mgombea wa urais wa CCM, ataendelea na kampeni, atakuwa Mkoa wa Pwani, ataenda Tanga, Kilimanjaro, Airusha, Manyara, Dodoma, mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan kwa sasa yupo Dar es Salaam na atakuwa kwa kazi za kiserikali kisha ataelekea Zanzibar ambako atafanya kampeni Unguja na Pemba, kisha ataenda Morogoro.

“Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa, kwa sasa yupo Dar es Salaam kwa kazi za kiserikali, ataenda mkoani Lindi na Mtwara kufanya kampeni, kwa kweli tumejipanga kuushangaza ulimwengu kwa ushindi wa kishindo," alitamba Polepole.

Polepole pia aliwataka wanachama wa chama hicho kuendelea kufanya kampeni za kistaarabu pamoja na kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kumchagua Dk. Magufuli kuendelea kuongoza nchi.

Vilevile, aliwataka wanachama wa CCM baada ya kupiga kura siku hiyo, warudi nyumbani na kusubiri matokeo aliyoyaita ya kishindo atakayopata mgombea wao huyo.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), pamoja na hukumu iliyotolewa na mahakama, mwananchi akishapiga kura, anatakiwa kuondoka katika kituo cha kupigia kura, wanaoruhusiwa kubaki ni mawakala wa vyama vya siasa pamoja na wasimamizi wa uchaguzi.

“Ushindi wetu kwa mwaka huu utakuwa mkubwa na haujawahi kutokea, mtaji wetu ni mkubwa sana. CCM kwa sasa tupo milioni 17, mtaji wetu wa ushindi ni asilimia 90,” alitamba Polepole.

Alisema kwa miaka mitano, Dk. Magufuli amefanya mambo madogo kwa kuwa yatakayofanyika miaka mitano ijayo ni makubwa zaidi.

Polepole pia aliwaomba Watanzania kuendelea kudumisha amani na CCM itaendelea kuisimamia serikali katika kudumisha amani.

Alisema: "Amani ni jambo la muhimu, CCM itaisimamia serikali kwamba amani ya Tanzania iko imara na madhubuti wakati wote. Walinzi wa amani wa taifa hili ni wananchi wenyewe, asiwatishe mtu. Tanzania 'hatunaga' shari na mtu yeyote."

Habari Kubwa