Upinzani wataja rafu mpya uchaguzi serikali za mitaa

11Nov 2019
Gwamaka Alipipi
DODOMA
Nipashe
Upinzani wataja rafu mpya uchaguzi serikali za mitaa

LICHA ya Serikali jana kuwaruhusu wagombea wa vyama vyote waliochukua na kurudisha fomu washiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, upinzani bungeni wameibuka na hoja mpya.

Mbunge wa Mtwara Mjini ( Cuf), Maftah Nachuma.

Akizungumza leo Novemba 11,2019 bungeni mjini Dodoma, Mbunge wa Mtwara Mjini ( Cuf), Maftah Nachuma amesema kuna wagombea zaidi ya asilimia 97 wilayani Liwale ambao wameshindwa kurudisha fomu baada ya kukuta ofisi za wasimamizi zimefungwa.

Amesema kuna idadi kubwa ya  wagombea mkoani Mtwara wameshindwa kurudisha fomu kwa sababu ya figisu figisu mbalimbali, lakini Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo hajawazungmzia watu hao bali amewataja waliofanikiwa kurudisha tu.

Jana Waziri Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodona amewataka wasimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa kuwaruhusu wagombea wote waliochukua na kurudisha fomu washiriki kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.

"Wilaya ya Liwale  mheshimiwa Spika zaidi ya asilimia 97 ya wagombea hawajarudisha fomu kwa sababu wamekuta ofisi za wasimamizi zimefungwa, sasa jana Waziri Jafo ametoa kauli kwa wagombea waliorudisha fomu watashiriki uchaguzi, vipi kuhusu walioshindwa kurudisha kwa kukuta ofisi zimefungwa?," amehoji Nachuma.

Kwa upande wa Mbunge wa Iringa Mjini ( Chadema), Mchungaji Peter Msigwa naye amesema eneo la Gangilonga jimboni kwake wasimamizi wa uchaguzi wamekimbia na kufunga ofisi hali iliyosababisha wagombea wengi wa upinzani kushindwa kurudisha fomu.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Jafo amesema wapinzani wanataka kuhamisha goli, kwamba hana majibu mengine zaidi ya yale aliyoyatoa jana.

Habari Kubwa