Upinzani kicheko, Mbowe, Matiko wakirejea uraiani

07Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Upinzani kicheko, Mbowe, Matiko wakirejea uraiani

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,  imetengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuwafutia dhamana Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, ambapo wameruhusiwa kuwa nje kwa dhamana.

Akitoa uamuzi huo mahakamani leo Alhamisi Machi 7, Jaji Sam Rumanyika, amesema Mahakama imekubali rufani hiyo kama ilivyo hivyo warufani wanatakiwa wawe nje na kwamba uamuzi wa kuwafutia dhamana ulifanyika mapema mno (pre mature).

“Aidha, sharti la kuripoti polisi kila alhamisi limefutwa badala yake watariporti mahakamani mara moja kwa mwezi si polisi tena kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Kisutu mara ya kwanza,” amesema.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwafutiwa Mbowe na Matiko dhamana kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana hiyo ambapo walikata rufaa Mahakama Kuu Desemba mwaka jana na uamuzi kutolewa leo.

Walifutiwa dhamana hiyo na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri Novemba 23, 2018 lakini siku hiyohiyo kupitia kwa wakili wao Peter Kibatala walikata rufaa Mahakama Kuu chini ya hati ya dharura sana wakipinga uamuzi huo.

Wakati huo huo Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imewaachia kwa dhamana wabunge wawili wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Susan Kiwanga (Mlimba) pamoja na Peter Lijualikali (Kilombero) baada ya kutupilia mbali madai ya Jamhuri. Mahakama imefikia uamuzi huo Mkoani Morogoro katika kesi ya msingi inayowakabili wabunge hao ambao wanatajwa kutenda kosa la jinai la kuanzisha vurugu na kuchoma mali za umma katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani Novemba 26, 2017

Akitoa uamuzi huo Hakimu Elizabert Nyembele amesema madai ya upande wa Jamhuri hayakuwa na msingi hivyo mahakama imeamua kuwapa dhamana washtakiwa.

Habari Kubwa