Uporaji wawatupa vijana jela miaka 30

03Sep 2017
Ibrahim Yassin
Nipashe Jumapili
Uporaji wawatupa vijana jela miaka 30

WAFUNGWA Paul Michael (20) na Lack Sichimata (19) wakazi wa Tunduma wilayani Momba mkoa wa Songwe,wameanza maisha ya kifungo cha miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa kutumia silaha.

Walihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Mbozi, Alhamisi wiki hii na Hakimu James Mhanusi, alisema kuwa ametoa adhabu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.

Awali wakisomewa shitaka hilo mahakamani hapo na mwendesha mashitaka Saro Mbele walidaiwa kutenda kosa hilo Machi 10, 2017, huku wakijua kufanya hivyo ni kosa na kinyume cha sheria za nchi.

Saro, alisema siku hiyo washitakiwa hao walivamia maeneo mbalimbali ya biashara katika mji wa Tunduma kisha kuiba mali mbalimbali baada ya kuvunja na kutumia silaha za moto ambazo hata hivyo hawana kibali cha kuzimiliki na kuzitumia.

Aidha washitakiwa walipopewa nafasi ya kujitetea mahakamani hapo waliiomba mahakama iwaonee huruma kwa kuwaachia huru au kuwapa kifungo kidogo kwani wanategemewa na familia zao. Maombi hayo yalitupiliwa mbali na mahakama hiyo.

Baada ya utetezi huo, hakimu aliamuru wakatumikie jela miaka 30 ili iwe fundisho kwa watu wengine, wenye tabia kama hizo ambao wanataka kujipatia mafanikio kwa njia za wizi, ujambazi na mauaji.

Nje ya mahakama, baadhi ya watu waliohudhuria mahakamani hapo, wamepongeza mahakama hiyo kwa kutoa hukumu hiyo, wakisema vijana hao walikuwa tishio katika mji wa Tunduma na maeneo mengine ambapo walikuwa wakiendesha unyang’anyi kwa kutumia siraha.

Waliongeza kuwa mji wa Tunduma ni wakibiashara,hivyo wafanyabiashara walikuwa wakilazimika kufunga mapema biashara zao wakihofu kuporwa na kwamba hukumu hiyo itawafanya wale wengine wenye tabia kama hiyo waogope.

Habari Kubwa