Usafiri wa meli Ziwa Victoria kuanza rasmi Agosti 16

14Aug 2020
Rose Jacob
Mwanza
Nipashe
Usafiri wa meli Ziwa Victoria kuanza rasmi Agosti 16

SIKU chache baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Agosti 9, mwaka huu, kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Leonard Chamuriho, kuhakikisha kibali cha meli ya New Victoria Hapa Kazi Tu, kinapatikana ndani ya siku mbili, hatimaye kimetolewa na meli hiyo itaanza huduma kwa wakazi wa Mwanza ...

na Bukoba, Jumapili hii.

Ratiba hiyo ilitangazwa rasmi Agosti 12, mwaka huu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa huduma za meli, Eric Hamissi.

Alisema, meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 200 za mizigo, itakuwa ikifanya safari za Mwanza kuanzia saa 3:30 usiku kupitia Kemondo ikielekea Bukoba na kufika saa 12:00 kamili asubuhi, mkoani Kagera.

Eric alisema katika hatua hiyo pia meli ya New Butiama Hapa Kazi Tu, yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 za mizigo, itaanza safari zake rasmi tarehe itakayotajwa na itatoka Mwanza kuelekea kisiwani Ukerewe.

"Meli hizo mbili zitaanza safari zake rasmi, kufuatia kukamilika kwa ukarabati na tayari zimeishakaguliwa na Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), kupewa vyeti vya ubora, baada ya mkandarasi KTMI Co. Ltd., ya Korea Kusini kumaliza shughuli hiyo, ambayo imegharimu Sh. bilioni 27.61 ikiwa ni fedha zilizotolewa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100," alisema Eric.

Kuanza kwa safari ya meli hizo kutasaidia kupunguza kwa adha za gharama za usafiri ikiwa na punguzo la bei ya ubebaji wa mizigo na tani moja mteja atalipa Sh. 27,000, Meli ya New Victoria ambayo itakuwa na madaraja matatu tiketi zitauzwa kwa Sh. 16,000 kwa daraja la uchumi, daraja la biashara 30,000 na daraja la kwanza 45,000, huku meli ya New Butiama ambayo itakuwa na madaraja mawili tiketi zikiuzwa kwa Sh. 8,000 kwa daraja la uchumi na 10,000 daraja la biashara.

"Meli ya New Victoria ilisimama kutoa huduma ya usafiri tangu Desemba 2014, kwa sasa itakuwa ikifanya safari zake mara tatu kwa wiki kutoka Bandari ya Mwanza Kaskazini kila siku ya Jumapili, Jumanne na Alhamisi saa 3:30 usiku na kuwasili siku inayofuata alfajiri katika Bandari ya Bukoba kupitia Kemondo," alisema Eric.

Vile vile, kuhusu Meli ya New Butiama, kwa sasa itakuwa ikiondoka Bandari ya Nansio kila siku saa 2:00 asubuhi na kuwasili Mwanza saa 4:00 asubuhi na itaondoka Mwanza saa 9:00 alasiri, itafika Nansio 11:00 jioni.

Habari Kubwa