Usafiri wa treni Katavi kwenda Tabora wasimama, reli yajaa maji

30Mar 2020
Neema Hussein
KATAVI
Nipashe
Usafiri wa treni Katavi kwenda Tabora wasimama, reli yajaa maji

Usafiri wa treni kutoka mkoani Katavi kuelekea mkoani Tabora umezuiliwa kwa muda kutokana na daraja linalopita katikati ya Mto Ugala kusombwa na maji  na kupelekea reli kufunikwa. 

hali hiyo imesababishwa na mvua inayoendelea kunyesha katika mkoa huo nakupelekea mto huo kujaa maji.

Wakizungumza na Nipashe leo Machi 30, 2020 wakazi wa Mkoa wa Katavi wamesema usafiri wa treni ndiyo uliyokuwa umebaki kwa wananchi wa kipato cha chini pia ulikuwa ukitegemewa baada ya barabara ya usafiri wa mabasi kutoka Katavi kwenda Tabora kufungwa kutokana na Daraja la Koga kujaa maji.

"Yani kipindi hiki usafiri umekuwa shida sana, usafiri tuliyokuwa tunautegemea ni usafiri wa treni uliyokuwa umebaki pia nauli yake ilikuwa ndogo sasa hivi nayo imezuiliwa," wamesema wakazi hao.

Abubakari Juma ni Mkuu wa Kituo cha Treni, Ugala amekili kuzuiwa kwa usafiri huo kwa muda usiojulikana na kueleza kuwa tayari mafundi wapo eneo la tukio kutatua tatizo hilo.

" Ni kweli usafiri wa treni umezuiliwa kwa muda kutokana na Mto Ugala kurika maji na kupelekea daraja kusombwa ila mafundi wapo eneo la tukio wakitatua tatizo hilo," amesema 

Njia pekee ya usafiri kwa wananchi wa katavi kwa sasa ni usafiri wa anga au kusafiri kwa basi kupita  wilayani uvinza mkoani kigoma.

Habari Kubwa