Ushauri watolewa kudhibiti bidhaa bandia

22May 2019
Mary Geofrey
DAR
Nipashe
Ushauri watolewa kudhibiti bidhaa bandia

NCHI za Afrika Mashariki zimeshauriwa kushirikiana kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti bidhaa bandia ambazo zinaingia sokoni kwa asilimia 40.

Mwenyekiti wa Tume ya Kupambana na Bidhaa Bandia nchini Kenya (ACA), Flora Mtahi.

Ushauri huo, ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Tume ya Kupambana na Bidhaa Bandia nchini Kenya (ACA), Flora Mtahi, wakati akizungumza katika mkutano wao na Tume ya Ushindani (FCC) katika ziara yao ya kujifunza nchini.

Alisema nchi moja moja haziwezi kudhibiti uingiaji wa bidhaa bandia sokoni hali ambayo inasababisha kuendelea kuzunguka na kuendeleza kudidimiza uchumi.

"Tumekuja Tanzania kwa ajili ya kubadilishana mawazo na FCC na kuangalia namna ya kuboresha utendaji kazi wetu. Kikubwa tunachoweza kufanya kama nchi zinazoendelea katika kudhibiti uingiaji wa bidhaa zisizo na ubora sokoni ni kuunganisha nguvu ya pamoja kwa kuwa na sheria zitakazosimamiwa na kuwa na mipango ya pamoja," alisema Mtahi.

Alifafanua kuwa asilimia 40 ya bidhaa bandia zinaingia sokoni katika nchi za Afrika zinasababisha kudhoofisha ukuaji wa uchumi wa nchi hizo.

Aidha, alisema kuwapo kwa bidhaa zisizo na ubora sokoni kunasababisha kufukuza wawekezaji kwenye nia ya dhati ya kutengeneza bidhaa zenye ubora.

Mwenyekiti wa FCC, Humfrey Moshi.

Naye Mwenyekiti wa FCC, Humfrey Moshi, alisema wanasimamia suala la bidhaa bandia kwa kuzuia uingiaji wake kuanzia bandarani, kudhibiti kuingia dukani, kuwanyang'anya wauzaji na kuwatoza faini.

Alisema changamoto kubwa katika sekta hiyo ni uelewa mdogo kutoka kwa watumiaji wa bidhaa hizo kwa sababu ya Watanzania wengi hupenda kununua bidhaa za bei nafuu badala ya kuzingatia ubora.

Alisema kuendelea kuingia kwa bidhaa hizo kunachangia kwa kiasi kikubwa kukimbiza wawekezaji wenye nia njema na kusababisha madhara ya afya kwa watumiaji.

Mmoja wa wawakilishi kutoka Wakala wa Kudhibiti Ushindani nchini Kenya akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushirikiano na Tanzania katika kudhibiti bidhaa bandia zinazoingia sokoni.

Habari Kubwa