Usiyoyajua kuhusu Airbus A220-300 inayotua leo Dar

11Jan 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Usiyoyajua kuhusu Airbus A220-300 inayotua leo Dar

RAIS John Magufuli, leo anatarajiwa kuwaongoza mamia ya wananchi katika mapokezi ya ndege nyingine mpya aina ya Airbus yenye muundo wa A220-300.

Aina hiyo ya ndege ni ya pili baada ya kupokea nyingine ya aina hiyo Desemba 23, mwaka jana, zote zikiwa zimenunuliwa na serikali kwa ajili ya kuboresha usafiri wa anga.

Kununuliwa kwa ndege hizo ni mwendelezo wa jitihada za serikali ya awamu ya tano ya kuimarisha usafiri wa anga nchini baada ya kununua ndege aina ya 787-8 Dreamliner iliyopewa jina la Kilimanjaro.

Ndege zote hizo zinanunuliwa na serikali na kukodishwa kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Ndege ya Airbus iliyowasili nchini Desemba 23, mwaka jana, ilipewa jina la Dodoma ikiwa na nembo ya 'Hapa Kazi Tu', lakini inayowasili leo imepewa jina la Ngorongoro ambayo nayo ina nembo ya hapa ‘Hapa Kazi Tu’.

Hapa Kazi Tu imekuwa kaulimbiu ya Rais Magufuli tangu wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Mambo muhimu kuhusu Airbus A220-300.

Ndege ya Airbus ina urefu wa mita 38.7 na kwa jumla inaweza kupakia abiria 141.

Urefu wake kutoka chini kwenda juu ni mita 11.5, na upana wa mabawa yake ni mita 35.1.

Airbus 220-300 inaweza kusafiri umbali wa kilometa 5,920 kwa safari moja bila kutua na inaweza kupaa ikiwa na uzito wa tani 67.6 na kutua ikiwa na uzito wa tani 58.7.

A220-300 ndiyo ndege kubwa miongoni mwa ndege za familia ya A220 na iliundwa kulenga soko la safari za ndege zinazowabeba abiria kati ya 130-160.

Ni ndege ambayo imetengenezwa kupunguza gharama ya matumizi ya mafuta kwa kila safari na pia kuwa yenye uwezo wa juu.
Injini zake zimepunguza matumizi ya mafuta kwa kila abiria kwa asilimia 20 ukilinganisha na ndege nyingine.

Ndege za A220 zimejengwa kwa vipande vinavyoweza kutengenezwa kwa haraka kiwandani iwapo vitahitajika wakati wa ukarabati.

Injini zake pia huwa za aina moja na marubani waliozoea ndege aina ya A220-300 na A220-100 hawahitaji mafunzo zaidi kuweza kuziendesha.

Shirika la ATCL Tanzania

Shirika la Ndege la Tanzania kwa sasa lina ndege saba, baada ya kununuliwa ndege sita chini ya mpango wa kufufua shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1977.

Kuna Bombardier DASH8 Q400 tatu, mbili ambazo zilifika nchini Septemba 2016 na moja Juni 2017, Bombardier CS300 mbili na Boeing 787 Dreamliner ambazo zilitua kati ya Mei na Julai, mwaka jana.

Kabla ya ujio wa ndege hizo, ATCL ilikuwa na Bombardier DASH8 Q300 moja ambayo ilikuwa ikitumika tangu mwaka 2011.

Habari Kubwa