Usiyoyajua kuhusu Mwalimu Nyerere

14Oct 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Usiyoyajua kuhusu Mwalimu Nyerere

MWANASHERIA wa Kenya, Prof. Patrick Lumumba, amesema waasisi wa Afrika akiwamo Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, walilenga kujenga mataifa ambayo yatakuwa na umoja wa kujiendeleza kisiasa, kiuchumi na kudumisha amani.

Prof. Lumumba aliyasema hayo jana wakati wa kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililofanyika mjini Chato mkoani Geita na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.

Akizungumzia demokrasia, Prof. Lumumba alisema lazima wafahamu nchi za Afrika zilibuniwa na zile za Bara la Ulaya.

Alisema baada ya nchi za Afrika kushikwa na kutawaliwa kimabavu, wanaharakati katika nchi za kiafrika walijitolea kurejesha uhuru akiwamo Mwalimu Nyerere.

“Wakati ule wanaharakati hawa waliposhiriki katika vita dhidi ya vile vya kikoloni, nchi nyingi ambazo zilikuwa zinatawala hazikuwa na lengo la kuruhusu nchi za Afrika zijitawale, nchi mbalimbali zilikuwa na vita na watu wengi wakapoteza maisha.

“Hivi sasa tupo katika ukoloni mamboleo, tukiangazia suala la uhuru, tuna uhuru wa kisiasa, tuna wimbo wa taifa, bendera na kaulimbiu lakini katika nyanja ya uchumi bado tunaelekezwa kutoka nchi mbalimbali za Ulaya, China. Swali tunalojiuliza leo 'Je, demokrasia ni nini?”

Alisema Rais wa kwanza Ghana, Kwame Nkrumah aliwahi kueleza kuwa, mkoloni habadiliki ila anachofanya ni kubadilisha mbinu na hata akibadilika atahakikisha amewadhalilisha na kuwanyanyasa.

Pia alisema kiongozi huyo alisisitiza kuwa, Waafrika lazima watambue kwamba lengo litatimizwa tu ikiwa watajikinga na kujilinda na dhidi ya harakati hizo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alisema taifa ambalo halijui historia yake limefilisika, ni maskini na halina mtaji kwa sababu historia ya taifa ni kitu cha msingi.

“Tunatakiwa kuwa na wivu wa taifa letu, tusikubali taifa hili liondoke katika misingi hiyo iliyoachwa na waasisi wa taifa letu,” alisema.

Aliyewahi kuhudumu kama waziri katika serikali ya awamu ya kwanza na nafasi nyingine ikiwamo kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Getrude Mongela, alisema wanamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa raha na majonzi wameweka pembeni.

“Nguvu niliyonayo inatokana na malezi kutoka wa wazazi wangu, jamii niliyokulia, kutoka kwa wenzangu niliokutana nao katika maisha na kutoka kwenye kushirikiana na binadamu wenzangu ndani na nje ya taifa,” alisema.

*Soma zaidi kujua mambo mengi usiyoyafahamu kuhusu Mwalimu Nyerere ukurasa wa 11, 12, 13 na 14.

Habari Kubwa