Uswisi yazijaza asasi mabilioni

23Mar 2019
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Uswisi yazijaza asasi mabilioni

UBALOZI wa Uswisi nchini kupitia Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC), umezindua awamu ya tatu ya programu kwa ajili ya kuziwezesha asasi za kiraia kuboresha uwajibikaji.

Uswisi ina nia ya kuchangia zaidi katika kuimarisha utendaji kazi na uwajibikaji wa mamlaka za umma ili zitoe huduma bora kwa wananchi.
 
Hayo yalisemwa jana mjini Dodoma na Balozi wa Uswisi nchini, Florence Tingly, kwamba katika mpango huo SDC itachangia Sh. bilioni 18 kwa miaka minne ijayo kwa asasi kadhaa za kiraia ikiwa ni pamoja na Foundation for Civil Society (FCS), Policy Forum na Twaweza.
 
Alisema Ubalozi wa Uswisi unashirikiana na asasi hizo zinazohusika na uanzishwaji na usimamizi wa sera za maendeleo ili kuboresha maisha ya mwananchi wa kawaida.
 
Pia alibainisha kuwa Uswisi inaamini kwamba asasi za kiraia ni moja ya wadau muhimu kwa nchi ya Tanzania ili kufikia malengo yake kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025. 
 
Alisema Uswisi tayari ina ushirikiano wa muda mrefu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika kuimarisha uwezo wake wa uchunguzi.
 
Aliongeza kuwa pia inachangia mpango wa utawala bora wa fedha  unaotekelezwa na Shirika la Ujerumani (GIZ0 na kwamba hiyo inafanya kazi ya kuzijengea uwezo na kutoa msaada wa kiufundi kwa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani na halmashauri za wilaya.

Habari Kubwa