Utafiti wafichua siri uzazi mpango, maambukizi VVU

17Jun 2019
Elizaberth Zaya
DAR
Nipashe
Utafiti wafichua siri uzazi mpango, maambukizi VVU

UTAFITI uliofanywa na muunganiko wa magwiji wa utafiti Duniani kuangalia endapo kuna uhusiano wa kupata Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa mwanamke anayetumia njia za uzazi wa mpango (ECHO), umebaini kwamba hakuna uhusiano wa kupata maambukizi hayo kwa kutumia njia za hizo za uzazi wa mpango.

Utafiti huo wa kubaini uhusiano wa maambukiz hayo ya VVU na matumizi ya njia za uzazi wa mpango umechukua muda wa miaka minne kukamilika kuanzia mwaka 2015 hadi Desemba 2018 na kutolewa rasmi Juni 14 mwaka huu na ulifanywa kwa kuangalia maambukizi hayo kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwamo Kenya, Eswatin na Afrika Kusini.

Akizungumza katika semina ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa na Inter News mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuwajengea uwezo juu ya utafiti huo na masuala mengine ya afya, Mhamasishaji jamii wa VVU na afya ya Uzazi, Dk. Lilian Mwakyosi, alisema utafiti huo ulihusisha njia za uzazi wa mpango za sindano, kitanzi na kipandikizi.

Alisema utafiti huo ulifanyika baada ya kuwapo kwa wasiwasi mkubwa wa kupata VVU kwa wanawake wanaotumia njia hizo za uzazi wa mpango kwa miaka mingi.

“Kwa muda mrefu kuna watu walikuwa wanahisi na kuuliza maswali kwamba labda kuna uhusiano baina ya kutumia njia za uzazi wa mpango na kuongezeka kwa hatari ya kupata VVU, kwa hiyo ilibidi jopo la watafiti kutoka katika nchi mbalimbali duniani wafanye utafiti huo, na waliamua kufanya kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa sababu maambukizi yalikuwa juu katika nchi hizo na waliangalia katika njia za uzazi wa mpango za kitanzi, sindano na kipandikizi,”alisema Dk.Mwakyosi.

Aliongeza: “Na waliangalia kwa wanawake walio katika uwezekano wa kupata ujauzito kuanzia miaka 16 hadi 30.”

Kuhusiana na kundi la watu ambao wanaongoza kwa maambukizi mapya ya VVU, Dk. Mwakyosi alisema katika utafiti huo, imebainika kuwa wanawake ndiyo wanaongoza kwa kwa kupata maambukizi hayo japokuwa maambukizi wanayopata hayahusiano na matumizi hayo ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

“Kundi la wanawake ndiyo linapata maamukizi mapya ya VVU kuliko kundi jingine kwa sababu katika utafiti huo inaonyesha kuwa hata katika kundi la watu 100 nusu ya watu wanaofanyiwa utafiti, nusu ya hao waathirika ni wanawake ingawa maambukizi haya hayahusiani kabisa na matumizi ya njia za uzazi wa mpango,”alisema Dk. Mwakyosi.

Aliongeza: “Na ndiyo maana tunashauri kwamba kuna haja ya kuendelea kubuni njia mbalimbali za kuzuia maambukizi haya na siyo kwa kutegemea Kondomu pekee, hatutakiwi kupuuza na kuona maamukizi haya yakiendelea kwa wanawake.”

Habari Kubwa