Utafiti waiweka matatani Twaweza

12Jul 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Utafiti waiweka matatani Twaweza

TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), imetoa siku saba kwa shirika lisilo la kiserikali la Utafiti la Twaweza lijieleze kwa nini lisichukuliwe hatua za sheria kutokana na kutoa utafiti bila kupata kibali.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu.

Kwa mujibu wa barua yake ya Julai 9, ambayo ililiandikia shirika hilo, Costech imetoa siku saba ambazo zilianzia Jumatatu na zinatarajia kuishia Jumapili.

Costech ilithibitisha jana kuwa barua hiyo ni yao na waliwaandikia Twaweza na kushangaa kwanini imesambazwa katika mitandao ya kijamii.

Baada ya Nipashe kutaka ufafanuzi wa barua hiyo kutoka Costech, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilituma maelezo kuwa leo Julai 12 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume atatolea ufafanuzi suala hilo.

“Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Costech atazungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Tume kutolea ufafanuzi kuhusu barua hii inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosambaa mitandaoni jana, Costech ndicho chombo chenye mamlaka ya kisheria katika kushauri na kusimamia masuala yote yanayohusiana na sayansi, teknolojia na ugunduzi.

Aidha, barua hiyo ilieleza kuwa Costech ndio wenye mamlaka ya kutoa kibali na kuruhusu kufanyika kwa utafiti au stadi mbalimbali za masuala ya sayansi na teknolojia zinazofanyika nchini.

“Costech ndio taasisi yenye mamlaka ya kutoa kibali na kuruhusu kufanyika kwa utafiti au stadi mbalimbali za masuala ya sayansi na teknolojia zinazofanyika Tanzania,” ilieleza barua hiyo.

Aidha, barua hiyo ilieleza kuwa kwa mujibu wa kumbukumbu zao, inaonyesha kuwa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza iliomba kibali cha kufanya utafiti kwa ajili ya maeneo manne.

Taarifa ya Costech ilieleza kuwa Twaweza lilikamilisha utafiti wao katika eneo moja na walikuwa wamebakiza maeneo matatu.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kulikuwa na taarifa ya matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza uliokuwa na kichwa cha habari kinachosema ‘Sauti za Wananchi’.

Utafiti huo pamoja na mambo mengine, ulibaini kuwa karibu wananchi wote wanafahamu vyama vikuu vitatu vya siasa nchini.

Wananchi walionyesha kufahamu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa asilimia 100, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa asilimia 97 na Chama cha Wananchi (CUF) kwa asilimia 83.

Kwa upande wa vyama vingine vya siasa National Convention for Construction and Reform (NCCR Mageuzi) asilimia 54 kinajulikana zaidi kikifuatiwa na Tanzania Labour Party (TLP) asilimia 41 na ACT-Wazalendo kwa asilimia (32).

Utafiti huo ulionyesha jamii inavifahamu vyama vikubwa vya siasa na kwa upande wa vyama vidogo vinafahamika zaidi miongoni mwa wanaume, vijana, wananchi wenye uwezo wa kifedha na wakazi wa maeneo ya mijini.

“Katika kumbukumbu zetu hatujawahi kupokea taarifa ya maombi ya Twaweza ya kuomba kibali cha kufanya utafiti huu na kitendo cha kusambaza taarifa ya utafiti huu ni uvunjaji wa sehemu ya 11 ya Kanuni za Muongozo wa Taifa wa Kuidhinisha Kufanya Utafiti,” ilieleza.

Kutokana na hali hiyo katika barua hiyo, Costech imetoa siku saba kwa Twaweza kujieleza kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yao baada ya kuvunja mwongozo huo wa taifa wa kuidhinisha masuala ya utafiti.

 

Habari Kubwa