Utakatishaji fedha wajadiliwa

15Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Utakatishaji fedha wajadiliwa

WIZARA ya Fedha na Mipango kupitia Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) imeandaa warsha kuhusu udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi kwa wadau wa sekta ya fedha.

Lengo la warsha ni kuendelea kuwakumbusha kuhusu umuhimu wa kulinda mfumo wa fedha wa nchi ili usitumiwe vibaya na wahalifu na watu wasio waaminifu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo juu ya udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi, Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Onesmo Makombe, alisema tatizo la utakatishaji wa fedha haramu ni tatizo kubwa ulimwenguni kote na katika jamii kwa sababu ya kuwapo kwa vitendo mbalimbali vya uhalifu vinavyowapatia wahalifu pato haramu.

Alisema uhalifu huo ni pamoja na ukwepaji kodi, biashara haramu ya dawa za kulevya, biashara haramu ya watu, biashara haramu ya silaha, rushwa, kughushi, ujangili, uharamia, uvunaji haramu wa magogo, uuzaji wa bidhaa bandia, ujambazi na uporaji.

Aidha, aliainisha madhara ya utakatishaji wa fedha haramu kuwa ni ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama. Madhara hayo pamoja na uhalifu kuendelea kushamiri kwa uhalifu na wahalifu kujiimarisha; wahalifu kuwa na nguvu kiuchumi; kuhatarisha utawala wa sheria na usalama, kutishia amani, utulivu na utawala wa sheria kwa kuwa uhalifu unaposhamiri na makundi ya uhalifu yanapojiimarisha hupata nguvu na kujaribu kudhibiti vyombo vya usalama au kushindana na vyombo vya dola.

Aliwaasa na kuwakumbusha washiriki kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kutekeleza wajibu wao wa kisheria kwa uadilifu na uaminifu ili kuendelea kusaidia katika kubaini wahalifu wanaoweza kutumia mfumo wa fedha wa nchi kutakatisha fedha haramu na kufadhili vitendo vya kigaidi na kuhatarisha usalama wa nchi.

Habari Kubwa