Utambuzi wamiliki wa nyumba uambatane na viwanja visivyolipiwa -Mabula

23Feb 2021
Dotto Lameck
Songwe
Nipashe
Utambuzi wamiliki wa nyumba uambatane na viwanja visivyolipiwa -Mabula

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, ametaka zoezi la utambuzi wa wamiliki wa nyumba liende sambamba na kutambua viwanja visivyolipiwa kodi ya pango la ardhi.

Dk. Mabula ametoa agizo hilo Jana wakati akizungumza na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Songwe pamoja na Watendaji wa Sekta ya Ardhi alipokuwa katika ziara ya siku moja ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi. 

Mabula amesema ni vyema zoezi hili la kutambua wamiliki wa nyumba linalosimamiwa na TAMISEMI kupitia watendaji wake wa mitaa na vijiji likaenda sambamba na kutambua viwanja ambavyo havilipiwi kodi pamoja na wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa mazoezi hayo yana lengo moja la kuingizia serikali mapato.

“Hakuna maana kuchukua kodi ya jengo na kuacha kodi ya kiwanja maana kodi zote hizo zina lengo la kukusanya mapato ya serikali yatakayosaidia katika kuendeshaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya kimkakati” amesema Dk. Mabula.

Amesema suala la utoaji hati katika Mkoa wa Songwe, Dk. Mabula ameoneshwa kutoridhishwa na kasi ya utoaji hati katika Mkoa huo ambapo katika kipindi cha miezi nane mkoa umetoa jumla ya hati 333 idadi ambayo amesema kuwa ni ndogo ukilinganisha na mikoa mingine na kutolea mfano wa Mkoa wa Mwanza katika Wilaya ya Ilemela kwamba watendaji wake wamejipanga ambapo kwa mwezi mmoja wanatoa jumla ya hati 350.

Habari Kubwa