Utata waibuka madai ya kukamatwa wakili maarufu

22Apr 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Utata waibuka madai ya kukamatwa wakili maarufu

BAADA ya taarifa kuhusu kutoweka kwa wakili na mwanaharakati Peter Madeleka, utata ulitanda kwenye mitandao ya kijamii huku chama cha ACT-Wazalendo kikieneza ujumbe wa hashtag#FreeMadeleka.

Peter Madeleka.

Katika ukurasa wa mtu anayetambulika kwenye mtandao wa kijamii tweeter, Hilda Newton, ilielezwa kuwa: ”Familia ya Madeleka wamefika Central Police (Kituo Kikuu cha Polisi) Dar muda huu kwa ajili ya kujua Madeleka kakamatwa kwa kosa gani lakini wameambiwa kwamba jeshi la polisi hawajamkamata wala hawamshikilii Madeleka.”

Msemaji wa ACT Wazalendo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarala Maharagande, kwenye ukurasa wake wa tweeter jana aliandika: “Jeshi la Polisi limtendee haki kwa mujibu wa Sheria Wakili Peter Madeleka kutokana na kumkamata kinyume cha taratibu na kutoruhusu ndugu wala wanasheria wake kuonana naye.”

Aidha Nipashe ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro, iwapo wanamshiilia wakili huyo, alisema: “Hapana, hatumshikilii. Kwa taarifa zaidi atafutwe kamanda wa mkoa wa Arusha”.

Kwenye ukurasa wa tweeter wa chama hicho ilielezwa zaidi kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika Hoteli ya Serena kwa watu wanaosadikiwa ni maofisa wa polisi wasio na utambulisho wowote na gari lisilo na namba za usajili wa polisi, walifika hotelini hapo na kumchukua wakili huyo bila kufuata taratibu za kisheria.

“Baadaye, baada ya ndugu na jamaa wa karibu kufuatilia, ndipo polisi walikiri kumshikilia. Siku za hivi karibuni, Wakili Peter Madeleka amekuwa akiishinikiza serikali kuwachukulia hatua maofisa wa Idara ya Uhamiaji waliofanya ubadhirifu wa utengenezaji wa stika feki za VISA kama ambavyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alivyobainisha kwenye taarifa yake ya ukaguzi wa 2020/2021,” ilisema taarifa hiyo.

“Tunataka Wakili Peter Madeleka apelekwe mahakamani ndani ya muda mfupi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi ili kuthibitisha kama kuna mashitaka dhidi yake,

Madai ya kukamatwa kwa wakili huyo yalizua taharuki baada ya kuvuja kwa taarifa za kundi la mtandao wa WhatsApp lililodaiwa kuwa la maofisa wa Uhamiaji kupanga mipango ya kumuua kwa kile kilichodaiwa anafichua siri za idara hiyo nyeti.

Habari Kubwa