Utata wajitokeza gharama karantini

25Mar 2020
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Utata wajitokeza gharama karantini

UTATA umeibuka kwa wasafiri kutoka nchi mbalimbali zenye maambukizo ya homa ya mapafu inayotokana na virusi vya corona (COVID-19), kushindwa kumudu hoteli walizopelekwa baada ya kuingia nchini.

Waziri wa afya Ummy Mwalimu, picha mtandao

Jana, ilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii, ikionyesha wasafiri zaidi ya 10 waliokuwa wakilalamika kuhusu gharama za hoteli walizopangwa na kwamba hakuna utaratibu maalum wa kuwahifadhi huku wakichanganyikana na watu wengine.

Vilevile, haijajulikana walikokwenda wageni hao baada ya uongozi wa hoteli walikopelekwa, kugoma kuwapokea na wenyewe kushindwa kumudu gharama hizo, huku usafiri uliotumika kuwapeleka hotelini kutoka uwanja wa ndege ukiondolewa eneo hilo la hoteli.

Katika video hiyo, mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake, alisema kuwa baada ya kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walipangwa kukaa kwenye hoteli ambazo gharama zake ni za kuanzia Dola za Marekani 55 kwa siku.

“Tulivyofika, tuliwaambia tukae nyumbani na tuwe tunakaguliwa, lakini kukawa na mabishano ya maneno ya kukaa hotelini tutakuwa tunakuja kukaguliwa wakaikataa, wakasema watatupeleka hotelini,” alidai.

Alizitaja hoteli walizotakiwa kwenda kuwa ni pamoja na Peacock, Rungwe, Southern Sun, Dar City Palace, Hot Reef na Lucky.

“Hizi ni hoteli ghali sana Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu na Waziri Ummy, hatuwezi kulipia kwa siku 14 na mnavyotuona tumebwagwa na hakuna mtendaji yeyote wa Wizara ya Afya na tayari tumekuwa hatarishi kwa watu tuliowakuta,” alisema dada huyo huku akiungwa mkono na wenzake.

Waliiomba serikali kuwasaidia kwa kuwa hoteli hizo ni ghali na bei zinaanzia Dola za Marekani 55 (Sh. 126,800), 78 (Sh. 179,800), 83 (Sh.191,400) na 105 (Sh. 242,100), huku kila hoteli ikiwa na kiwango chake cha kubadilishia dola kwa shilingi ya Tanzania.

Katika ukurasa wake wa Twiter jana, Waziri Ummy Mwalimu, aliandika huku akiambatanisha na video ya mwanamke huyo akilalamikia juu ya mahali pa kuhifadhiwa.

Waziri Ummy aliandika: “Tumepokea hii changamoto ya sehemu zilizobainishwa kwa ajili ya siku 14 za kijitenga kwa wasafiri waliotoka nchi zilizoathirika zaidi na COVID-19.

"Nawaelekeza Ma-RC (wakuu wa mikoa), RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) na DC (wakuu wa wilaya) zote kubainisha hoteli/sehemu ambazo wasafiri wengi watamudu gharama."

Nipashe iliutafuta uongozi wa Hotel ya Peacock na kuongea na Joel Mfugale, ambaye alikiri watu hao walifika hotelini kwao juzi na walivyowakataa, waliondoka na hawajui walikokwenda.

“Mkuu wa Wilaya alitangaza kuwa hoteli yetu ni moja ya hoteli itakayopokea watu hao, lakini sisi tulikataa kwa kuwa kwa wiki mbili inatakiwa hoteli isiwe na wageni wengine na wawapo madaktari au wataalamu wa afya, tulishindwa kuelewana,” alisema na kufafanua zaidi:

“Kuhusu bei kubwa, ilikuwa ni mpango wa mameneja ili tusiwapokee watu hao kutokana na kwamba hakuna maandalizi yoyote, na walivyoona hatuwapokei na waliowaleta (serikali) wameondoka, basi nao waliondoka na hatujui walielekea wapi.

“Sisi tuna wageni wengine, haiwezekani tukawa ‘quarantine’ (eneo la kujitenga) tutawahudumiaje wateja wetu? Na pia hakuna elimu yoyote iliyotolewa, ni ngumu na hatari sana kwetu kutunza watu hao."

Habari Kubwa