Utata zaidi sakata la faru John

10Dec 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Utata zaidi sakata la faru John
  • *Takukuru wajitosa kubaini kilichotokea
  • *Majaliwa akabidhiwa ripoti, pembe zake

SIKU nne tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kusema kuna harufu ya ufisadi katika kuhamishwa kwa faru John kutoka Kreta ya Ngorongoro kwenda Grumeti Mara, utata zaidi umeibuka sakata hilo.

Hali hiyo imeibuka baada ya jana mtendaji huyo mkuu wa serikali kupokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ikisema ilikuwa lazima mnyama huyo kuondolewa Ngorongoro.

Taarifa hiyo ambayo haikusema kama kulikuwa na suala la ufisadi katika kumhamishana faru huyo, ilisema baada ya faru huyo kukaa kwa muda alipohamishwa, afya yake ilidhorota na hatimaye kufa.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana, ilisema Majaliwa amepokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Profesa Maghembe alisema hadi Desemba, mwaka jana, wakati faru John anahamishwa, alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.

Kati ya faru 37 waliokuwapo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2.

Uamuzi wa kumwondoa John ulikuwa muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, alisema Waziri Maghembe.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Majaliwa alisema;Nilipokea taarifa yenu jana (juzi) saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo tukimaliza sherehe za maadhimisho ya Uhuru tukutane na kujadiliana kuhusu taarifa yenu.

Desemba 6, akiwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Majaliwa alisema faru huyo alitolewa kwenye hifadhi hiyo ili akauzwe Grumet kwa Sh. milioni 200.

Majaliwa alisema hadi kufikia siku hiyo alipokuwa akizungumza, tayari wahusika walishalipwa Sh. milioni 100 na watu wanaodaiwa kumnunua hivyo akamtaka Prof. Maghembe ampatie taarifa ya kina kuhusiana na faru huyo.

Nina taarifa kuwa mliiba faru John na kumpeleka VIP Grumeti Serengeti, Desemba 17, mwaka jana na badala yake mkapewa Sh. milioni 200, na mmepata mgawo wa Sh. milioni 100 halafu mnataka kusingizia kuwa amekufa. Yuko wapi faru John; alihoji akiwa katika ziara yake mkoani Arusha.

Awali, ilidaiwa kuwa faru huyo alihamishiwa Grumeti, eneo ambalo ni sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara, lakini likimilikiwa na raia wa kigeni aliyepewa kisheria kitalu hicho anachokitumia kwa shughuli za utalii.

Majaliwa aliagiza baadaye kuwa Waziri Maghembe awasilishe ofisini kwake leo taarifa za uhamishaji wa faru huyo pamoja na nyaraka ngumu (hard copy) zinazoonyesha vikao vya makubaliano ya kumhamishia huko.

Pembe za faru John Taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu ilisema akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande, alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.

Taarifa iliyotolewa jana iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru, inayoundwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.

Takukuru Kazini Taarifa ambazo gazeti hili ilizipata jana, zinasema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imejitosa kuchunguza suala hilo.

Hatua hiyo imedaiwa kufanya vigogo wengine tofauti na waliotajwa kwa majina na Waziri Mkuu kuwa kwenye wasiwahi wa kujumlishwa katika sakata hilo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kuhamishwa kwa mnyama kama huyo kuhusisha watu mbalimbali.

Licha ya taarifa ya taasisi hiyo kuingia kwenye suala hilo, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Wandwe Felix, alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu liko kwenye uchunguzi na sheria zinakataza kuzungumzia suala kama hilo.

Maswali Magumu Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili, James Lembeli, ndiye aliyeibua baadhi ya maswali ambayo majibu yake ni muhimu yakatolewa kupitia ripoti ya kuondoshwa kwa faru John, itakayokabidhiwa kwa Waziri Mkuu leo.

Lembeli alisema kwa namna yoyote ile, nyaraka atakazopewa Majaliwa zinapaswa kutoa majibu juu ya sababu za kuwapo kwa dalili za usiri wa jambo hilo.

Alisema eneo la Grumeti limegawanyika sehemu mbili, ambazo ni lile la uwindaji ambalo kuna mwekezaji amepewa kama la uwindaji, likiwa ni la idara ya wanyamapori; na pia kuna eneo jingine alinunua mwekezaji kama shamba lake na kuliunganisha na eneo la uwindaji.

Kwa sababu hiyo, Lembeli ambaye aliwahi kufanya kazi Tanapa kuanzia mwaka 1993 hadi 2005, aliongeza kuwa ni vyema wanaomwasilishia nyaraka Waziri Mkuu kuhusiana na kuondoshwa kwa faru huyo, wahakikishe wanaeleza vile vile kuwa ni wapi alikopelekwa faru huyo kati ya maeneo hayo mawili.

Lembeli alihoji ;Faru huyo alipelekwa wapi? Alihamishwaje?...alitembea kutoka Ngorongoro hadi akafika Serengeti na kuingia Grumeti au? Au alibebwa kwenye lori baada ya kuchomwa sindano au kupigwa risasi (maalum)?; Aidha, Lembeli alisema kazi ya kumhamisha faru kama John huhusisha watu wengi na vifaa maalumu na kwamba hilo ni jambo la kawaida, lakini muhimu zaidi ni kufuatwa kwa taratibu.

Nimeshangaa kusikia faru John niliyemfahamu kwa muda mrefu ameondoshwa (Ngorongoro)… lakini kusafirisha faru siyo jambo geni ikiwa litafanyika kwa uwazi.

Inapokuwa kwa siri ndiyo inaibuka harufu ya rushwa. Naona hapa kuna tatizo,; alisema na kuongeza;Kumtoa faru John Ngorongoro Crater na kumpeleka Grime maana yake amevuka Serengeti.

Ni umbali wa kilomita 100. Najiuliza alitembea, aliswagwa au alipakizwa kwenye gari?alihoji.

Alihoji pia kama Watanzania walijulishwa juu ya kuhamishwa kwa faru huyo na kwamba, miongoni mwa taratibu ni pamoja na kuwahusisha madaktari wakati wa kuhamishwa huko ili kulinda afya ya mnyama husika.

Alisema kama taratibu zilifuatwa, Kamati ya Bunge inayohusika na masuala ya maliasili ingekuwa na taarifa na kama lilifanyika baada ya hapo, ni lazima kufuatilia kwa undani kwa nini ilifanyika hivyo.

Kwa mujibu wa Lembeli ambaye amekuwa bungeni kwa miaka 10 huku miaka mitano ya mwisho akiwa mwenyekiti wa kamati, uamuzi huo ungefanyika wakati akiwa kwenye kamati, Wizara ingewajibika kuitaarifu kamati. ;Lazima kuna namna hapa hakukuwa na Serikali ya awamu ya tano.

Walifanya wakati hakuna Waziri.

Watueleze kibali kilitolewa na nani kwa wakati huo? Lakini nijuavyo, siyo jambo la dharura; naona walitumia mwanya wa kutokuwapo Serikali kamili kufanya haya, alisema.

Mmoja wa wadau wa utalii nchini, Aloyce Kimaro, ambaye amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Vunjo, alisema faru hulindwa kwa kutumia kompyuta na maisha yao hujulikana kirahisi.

Habari Kubwa