Utegemezi wahisani sasa asilimia nane

06Jul 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Utegemezi wahisani sasa asilimia nane

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema kiwango cha utegemezi kutoka kwa wahisani na washirika wa maendeleo katika bajeti kimepungua kutoka asilimia 12.5 mwaka 2017/18 hadi asilimia nane 2019/20.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa

Sambamba na hilo, amesema serikali itaendelea kuzingatia ombi la viongozi wa kidini kutafuta suluhu ya mambo mbalimbali ya maendeleo bila kuathiri Katiba ya nchi. 

Majaliwa aliyasema hayo jana alipomwakilisha Rais John Magufuli kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 53 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ulioambatana na hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa kitegauchumi cha jumuiya hiyo, jijini hapa.

Alisema serikali imeendelea kupunguza kiwango cha utegemezi kwa kuwa ndio msingi wa uongozi wa Rais Magufuli wa kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

"Kuimarika huko kwa bajeti yetu kunakwenda sambamba na kuimarika kwa huduma za kijamii kama vile elimu, maji na kupungua kwa umaskini wa mahitaji muhimu."alisema

Waziri Mkuu aliipongeza CCT kwa kuanza kuchukua hatua za kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea kiuchumi kwa kuwa zinahitajika nguvu za pamoja katika kuhakikisha wanawahudumia Watanzania na kuwaletea maendeleo. 

"Kujizatiti kwa CCT katika kufikia malengo yake ya kujitegemea kiuchumi ni muhimu katika kutimiza kusudio na agizo la Mungu la kuwahudumia wahitaji ambao ni Watanzania lakini pia mtakuwa mnajaliza juhudi za Serikali katika wajibu wake wa kuwahudumia wananchi,"alisema.

Majaliwa aliwataka viongozi wa dini waendelee kuimarisha malezi na mafundisho ya kiroho kwa vijana na kuepusha mmomonyoko wa maadili ili Taifa liendelee kung'ara, kuheshimika na kusifika duniani kwa utulivu, amani na umoja. 

Alisema serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo CCT katika kutengeneza mustakabali mwema na ustawi wa familia kupitia mahubiri ya injili na malezi ya kiroho kwa waamini.

"Tunatambua mchango wa malezi ya kiroho katika ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla na mafundisho yake kwani yamesaidia kujenga watumishi wa umma ambao wamelelewa katika misingi bora ya kumcha Mwenyezi Mungu," alisema.   

Waziri Mkuu alisema serikali inaamini kwamba watumishi wa namna hiyo watachapa kazi kwa bidii, uadilifu, uaminifu na kupiga vita vitendo vyote vya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma. 

Katika hafla ya uchangishaji fedha, Sh. milioni 357.35 zilipatikana na Waziri Mkuu alisema ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa CCT wa miaka mitano (2017 – 2022) wenye lengo la kuiwezesha CCT kujitegemea kwa kuwa na vitegauchumi vyake ambavyo vitaiwezesha kujiendesha kwa asilimia 80.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za CCT na madhehebu mengine ya dini katika kuwahudumia Watanzania kupitia sekta za elimu, maji, afya na shughuli za ujasiriamali.

Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Canon Matonya, alisema jumuiya hiyo imeanzisha mkakati wa kuwa na vitega uchumi vyake kwa lengo kuondokana na utegemezi wa fedha za ufadhili ambazo zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka.